1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malalamiko yanazidi dhidi ya serekali ya Iran

Miraji Othman29 Desemba 2009

Serekali ya Iran iko katika mbinyo

https://p.dw.com/p/LGSm
Michafuko kutokana na maandamano ya wapinzani wa serekali ya Iran mjini TehranPicha: AP

Mji mkuu wa Iran, Tehran, bado haujatulia tangu vurumai kuzuka wakati wa mazishi ya aliyekuwa kiongozi mkuu wa kidini na mkosoaji wa serikali, Ayatolla Hossein Ali Montazeri. Hii leo Maelfu ya waandamanaji wanaoiunga mkono serikali ya Iran chini ya uongozi wa rais Mahmoud Ahmadinejad, waliandamana kupinga maandamano na makabiliano baina ya polisi na wafuasi wa upinzani. Wafuasi hao waliobeba mabango waliwakashifu viongozi wa upinzani kwa kile walichotaja kama kudhalilishwa kwa hadhi ya Iran katika safu ya kimataifa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la taifa la Iran, waandamanaji hao pia wanataka wahusika wakuu kutoka upinzani wanaokisiwa kupanga maandamano dhidi ya serikali wachukuliwe hatua za kisheria.

Vyombo vya habari vya kimataifa pia vimekashifiwa kwa kushirikiana na kambi ya upinzani kusababisha hali ya taharuki na kutishia usalama wa nchi ya Iran inayozingatia sera zenye misingi ya kiislamu. Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad amekashifu maandamano yaliyopangwa na upinzani, akisisitiza kuwa ni njama ya kuzua rabsha inayoongozwa na Marekani na washirika wa Israel.

Awali balozi wa Uingereza nchini Iran, Simon Gass, alihojiwa na viongozi wa juu wa Iran kutokana na msimamo wa uingereza kuhusu mustakabali wa Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Manouchehr Mottaki, amesema Uingereza inafaa kukoma kuropoka na kuingilia maswala ya ndani ya Iran. Hata hivyo, serikali ya Uingereza imesimama kidete na kusisitiza kuwa haitatishika na kuketi pembeni kuhusu matukio ya kusikitisha nchini Iran.

Yamkini wanaharakati ishirini wa upinzani wamekamatwa tangu jumapili wiki iliyopita, wengi wao wakiwa waliotuhumiwa kuhusika katika vurumai yaliyotokea wakati wa maadhimisho ya sherehe ya kidini ya Ashura ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Kati ya waliokamatwa ni washauri wa ngazi ya juu katika kambi ya upinzani, akiwemo shemejiye Mirhossein Mousavi ambaye ni kiongozi wa upinzani.

Huku haya yakijiri, serikali ya Iran imetoa agizo la kukamatwa kwa washukiwa wanaopanga maandamano na kuwa polisi iwe chonjo dhidi ya wapinzani wa serikali na kuhakikisha kuwa hali ya utulivu inarejea.

Taarifa ya walinzi wa mapinduzi nchini humu inasema kwamba njama ya kudhalilisha ustawi wa serikali ni sawia na jitihada zitakazotumbukia nyongo na inadai kuwa ni wazi kwamba mashirika ya kigeni na vyombo vya habari vimeungana kutishia uhuru wa iran.

Sasa kumekuwa na Ubadilishanaji mkali ya maneno unayozua taswira ya kufokeana baina ya wafuasi wa serikali na wale wanaounga mkono kambi wa upinzani.

Takriban watu wanane wameripotiwa kuawa tangu kukithiri kwa maandamano na makabiliano huku baadhi ya maafisa wa polisi kujeruhiwa kwa kile serikali inataja kama uhasama unaoendelezwa na maadui wa serikali. Ebrahim Yazdi, ambaye ni katibu mkuu wa vuguvugu linalopigania uhuru na haki nchini Iran, amechangia kuwa kukamatwa kwa babake ambaye ni mpinzani, hakutakata kiu ya wa-iran kupigania demokrasia wala kupunguza sauti zao za kutaka haki. Tofauti na matukio na matamshi haya, spika wa bunge la Iran, Ali Larijani, ametoa wito kwa kitengo cha mahakama cha Iran kuimarisha mipango ya kuwakamata wanaohusika katika maandamano ya kupinga serikali kwa kile alichotaja kama matukio ya aibu na yenye kukejeli uhuru wa Iran. Maandamano yaliyopangwa kupinga kuchaguliwa tena kwa rais Mahmoud Ahmadinejad Juni 12 yalitajwa kama makubwa zaidi kuwahi kutokea kwa kipindi cha miaka 30 ya uhuru wa Iran.


Mwandishi- Peter Moss/AFP

Mhariri: Miraji Othman