1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya waasi yanatumia ghasia za kingono kusambaza hofu

Admin.WagnerD14 Aprili 2015

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema mwaka 2014 ulighubikwa na visa vya ubakaji, utumwa wa kingono na ndoa za lazima vilivyofanywa na wanamgambo wenye itikadi kali kuendeleza uasi wao.

https://p.dw.com/p/1F7UU
Nigeria Boko Haram Terrorist
Picha: picture alliance/AP Photo

Katika ripoti hiyo iliotolewa rasmi jana Jumatatu, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameelezea wasiwasi mkubwa alio nao kuhusu ghasia za kingono zinazofanywa na wanamgambo wa makundi yenye itikadi kali katika nchi za Iraq, Syria, Somalia, Nigeria Mali, Libya na Yemen.

Ban amesema nchi hizo zinazokumbwa na mizozo ambayo imechochewa kwa kiasi kikubwa na makundi yenye itikadi kali yamefichua kuwa wanamgambo hao wanatumia vitendo vya ghasia za ngono kama njia mojawapo ya kusambaza hofu na maovu yao dhidi ya raia.

IS na Boko Haram yatuhumiwa

Katibu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema juhudi za kuyaangamiza makundi kama ya IS, Boko Haram, Al Shabab, Ansar Dine na wanamgambo wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda ni sehemu muhimu ya vita dhidi ya ghasia za kingono katika nchi zinazokumbwa na mizozo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/dpa/Karim Kadim

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inaziangazia nchi kumi na tisa zinazokumbwa na mizozo au zinajaribu kujikwamua kutoka vita ambapo ubakaji, utumwa wa kingono, kulazimishwa kwa wasichana kuwa makahaba na kulazimishwa kubeba mimba zinatumika na wanamgambo dhidi ya wasichana na wanawake na vile vile maovu hayo ya kingono yanawakuta wavulana na wanaume.

Makundi 45 ya waasi na wanamgambo yameorodheshwa katika ripoti hiyo yakiwemo yaliko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ivory Coast, Congo, Iraq, Mali, Somalia, Sudan Kusini na Syria.

Umoja wa Mataifa umesema mojawapo ya visa ambavyo viliushutua ulimwengu mwaka jana, ni cha wasichana zaidi ya mia mbili wa shule waliotekwa nyara na waasi wa Boko Haram katika kijiji cha Chibok kaskazini mwa Nigeria.

Wasichana waozwa kwa lazima na waasi

Ripoti hiyo imeelezea kwa kina kuwa waasi hao wa Boko Haram mara kwa mara wanawateka nyara wasichana na wanawake na kuwalazimisha kuolewa au kuwabaka mara kwa mara. Wasichana waliotekwa nyara wanaokata kuozwa kwa lazima au kubakwa wamekuwa wakiteswa na kuuawa.

Wasichana wa Chibok waliotekwa nyara na Boko Haram mwaka 2014
Wasichana wa Chibok waliotekwa nyara na Boko Haram mwaka 2014Picha: picture alliance/AP Photo

Katika jimbo la Darfur nchini Sudan, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, idadi ya walioachwa bila ya makaazi imeongezeka sawa na idadi ya visa vinavyoripotiwa vya ghasia za kingono.

Katika nchi jirani ya Sudan Kusini, visa hivyo vinazidi kuongezeka vikiwemo magenge kuwabaka wanawake, kuwalazimisha kuwa uchi,kuwalazimisha kuavya mimba na kuwahasi wanaume.

Hata hivyo ripoti hiyo imesema ghasia za kingono zimepungua katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kufuatia juhudi zilizochukuliwa na serikali zikiwemo kuwafungulia mashitaka maafisa wa ngazi ya juu serikalini na kuwalipa fidia waathiriwa.

Mwandishi:Caro Robi/Ap

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman