1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano yafikiwa Kenya

Schmidt, Andrea DW 29 Februari 2008

Rais Mwai Kibaki wa Kenya na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamekubaliana kuunda serikali ya mseto.

https://p.dw.com/p/DFhs
Rais Mwai Kibaki na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga watia saini mapatano ya kuunda serikali ya msetoPicha: picture-alliance/ dpa

Wananchi wa kenya wameanza kuvuta pumzi ya faraja baada ya rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kufikia mwafaka juu ya kuunda serikali ya mseto na jumuiya ya kimataifa pia imeshangalia mwafaka uliofikiwa kutokana na juhudi za upatanishi za aliekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa bwana Kofi Annan.

Baada ya mazumguzo magumu ya miezi miwili rais mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamekubaliana kuunda serikali ya mseto ambapo bwana Odinga atakuwa waziri mkuu.

Yumkini mwafaka huo utamaliza mgogoro wa kisiasa ulioikumbuka Kenya kufuatia kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika desema mwaka jana.

Upande wa upinzani ulidai kwamba udanganyifu ulifanyika katika hesabu za kura.

Ghasia zilizofuatia zimesababisha vifo vya watu wapatao1500 na watu wengine zaidi ya laki tatu wamekimbia makao yao.

Kutokana na mgogoro wa kisiasa, uchumi wa Kenya uliokuwa unastawi vizuri ulishaanza kuathirika. Nchi jirani zinazoitegemea Kenya katika uingizaji na utoaji wa mizigo pia zimeathirika.

Ni hatua ya nadra kuona jumuiya ya kimataifa ikijihusisha moja kwa moja katika juhudi za kuleta suluhisho la mgogoro katika nchi ya kiafrika.


Lakini pamoja na juhudi za jumuiya ya kimataifa yafaa kutilia maanani kwamba,

upande wa upinzani ulikubali kuacha dai la kumtaka rais Mwai Kibaki ajiuzulu wakati serikali ilikuwa inajaribu kuhimili kila shinikizo la jumuiya ya kimataifa.

Makubaliano yaliyofikiwa juu ya kugawana madaraka baina ya serikali na upande wa upinzani ni fursa ya kurejesha demokrasia nchini Kenya.Chini ya mpango huo wadhifa wa waziri mkuu utaundwa: pongezi kwa bwana Kofi Annan.Kenya ilikuwa inakaribia kwenye ukingo wa vuramai.

Bwana Annan alianza juhudi za kuzipatanisha pande za serikali na upinzani tokea mapema mwezi janauri-amefanikiwa ,pia kutokana na kuungwa mkono na mwenyeikiti wa sasa wa Umoja wa Afrika,rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Muhimu sasa ni kuchukua hatua za kuunda serikali itakayokuwa na uwezo wa utekelezaji.Hali ya kutoaminiana baina ya rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga lazima sasa iondoke na badala yake yawekwe mazingira ya ushirikiano katika msingi wa kuamianina.

Hatahivyo wadadisi wanahofia kwamba wanasiasa wamekubaliana kuwagawana madaraka lakini wamepuuza kuzingatia matatizo na mizizi ya mgogoro iliyopaswa kushughulikiwa muda mrefu sana uiliopita-ikiwa pamoja na megeuzi muhimu katika nyanja za sheria,na uchumi, ambapo baadhi ya jamii,sehemu za nchi, na makundi fulani ya watu yanapunjika sana.


Yaliyotokea ,ikiwa pamoja na vifo vya watu1500 lazima yachunguzwe haraka iwezekanavyo kwa msaada wa tume ya maridhiano.

Hadi kuziba pengo baina ya jamii mbalimbali nchini Kenya, muda mrefu utahitajika lakini mageuzi lazima yafinyike ili kupiga vita rushwa na ili kuleta haki za kijamii ili kujenga Kenya imara.


Mtafsiri Abdu Mtullya.