1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya amani ya Kongo Magazetini

8 Novemba 2013

Mada iliyogonga zaidi vichwa vya habari vya ripoti za magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii inahusu kusalim amri waasi wa M23 mashariki ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na mataokeo yake.

https://p.dw.com/p/1AEIn
Rais Joseph Kabila wa Kongo
Rais Joseph Kabila wa KongoPicha: Reuters

Lakini pia mjadala wa wanasheria nchini Kenya kuhusu mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague umezingatiwa.

Tuanzie lakini na jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ambako wananchi wameanza kushusha pumzi baada ya kushindwa nguvu wanamgambo wa M23 katika eneo la mashariki la nchi hiyo.Kundi lililokuwa na nguvu kabisa mashariki ya Kongo limelazimika kuwapigia magoti wanajeshi wa serikali wakisaidiana na wale wa tume ya kulinda amani ya umoja wa mataifa, linaandika gazeti la Die Welt linalohisi hali hiyo imesababishwa zaidi na shinikizo la Marekani kwa serikali ya Rwanda.

Rais Paul Kagame daima amekuwa akikanusha madai kwamba nchi yake inawaunga mkono waasi wa M23,hata hivyo die Welt linasema kila kitu kinaonyesha kusitishwa ghafla misaada ya Rwanda kwa waasi ndio chanzo cha kushindwa M23. Lakini pia kuimarishwa vikosi vya Umoja wa mataifa vilivyoongezwa na kuwa wanajeshi 3000 pamoja na nidhamu katika jeshi la serikali ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuwashinda nguvu waasi,linaandika gazeti la Die Welt.

Gazeti la Süddeutsche linaandika "Ushindi lakini si amani".Baada ya kuelezea umuhimu wa kuvunjwa nguvu M23,mojawapo kati ya makundi yasiyojulikana idadi ya waasi katika eneo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,mhariri wa gazeti hilo la kusini mwa Ujerumani anasema mbali na kuwa ushindi kwa jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Umoja wa mataifa Monusco,ni ushindi pia kwa jumuia ya kimataifa akikumbusha mzozo wa mashariki ya Kongo daima ulikuwa ukitajwa kama "vita vya kwanza vya dunia barani Afrika.

Kamanda wa M23, Sultani Makenga
Kamanda wa M23, Sultani MakengaPicha: PHIL MOORE/AFP/Getty Images

"Hata hivyo hii ni hatua moja tu kuelekea amani katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,linanadika gazeti la Süddeutsche lililomnukuu mkuu wa tume ya Umoja wa mataifa nchini humo Martin Kobler akisema kuna makundi mengine yasiyopungua 48 yanayopigana katika eneo hilo.

Mhariri wa gazeti la Süddeutsche anajiuliza kama uamuzi wa kusalim amri M23 utadumu na kama ndio chanzo cha kupatikana amani katika eneo hilo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Frankfurter Allgemeine linaahisi pia kwamba M23 wameamua kusalim amri baada ya kukosa uungaji mkono kutoka Rwanda ambayo kwa upande wake imesitishiwa misaada kutoka Ulaya na Marekani.Baada ya kushindwa M23,rais Joseph Kabila ameahidi kuwaandama waasi wa FDLR,waliokimbilia Kongo baada ya mauwaaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994.

Ameaahidi mara nyingi linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine na kukumbusha ikiwa safari hii hatotekeleza ahadi yake,Rwanda itapata sababu ya kutopakata mikono. Uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague kuakhirisha kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta umechambuliwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.

Eti haki ni sawa kwa wote? linajiuliza gazeti la Der Tagesspigel linalozungumzia mabishano ya wanasheria wa Kenya kuhusu mahakama hiyo ya kimataifa mjini The Hague."Rais barani Afrika ni mtu muhimu na analinganishwa na mtemi"Linapohusika suala la hadhi ya rais,waafrika wengi wanakuwa wakali",linaandika gazeti la Der Tagesspiegel linalomnukuu mhadhiri wa kitivo cha sheria cha chuo kikuu cha Strathmore,Luis Franceschi akielezea kwanini Umoja wa Afrika katika mkutano wao wa dharura mjini Addis Abeba mwishoni mwa mwezi uliopita,umetamka marais walioko madarakani,mawaziri wakuu na mawaaziri wasifikishwe mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu kabala ya mhula wao kumalizika.

Muda mfupi kabla ya hapo mwanaharakati wa haki za binaadam wa Kenya Haron Ndubi aliuliza suala kwanini Umoja wa Afrika unapigania hadhi ya marais,lakini haufanyi chochote linapohusika suala la kutetea hadhi ya wahanga wa matumizi ya nguvu ya baada ya uchaguzi mwaka 2007. Hoja hizo linaandika gazeti la Der Tagesspiegel haziungwi mkono na balozi wa Ethiopia Fesseha Asghedom ambae nchi yake ndio mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou BensoudaPicha: AFP/Getty Images

Anahoji "juhudi za kusaka usawa hazistahiki kuhatarisha amani."Suala la waziri wa zamani wa sheria wa serikali kuu ya Ujerumani,Herta-Däubler-Gmelin wa kutoka chama cha Social Democrat kama hoja kama hizo haziurejeshi Umoja wa Afrika kufuata muongozo wa zamani wa "kutoingfilia mambo ya ndani ya nchi mwanachama ,hakulijibu balozi huyo wa Ethiopia anaandika Dagmar Dehmer wa der Tagesspiegel.

Na kwa ripoti hiyo ya Der Tagesspiegel ndio na sisi tunazifunga kurasa za yale yaliyoanadikwa na wahariri wa magazeti wa Ujerumani kuhusu bara la Afrika mnamo muda wa siku sabaa zilizopita.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ Basis/Presser/All Presse
Mhariri: Josephat Charo