Makampuni ya kuunda magari yahitaji msaada zaidi. | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Makampuni ya kuunda magari yahitaji msaada zaidi.

Mipango mipya ya kujinusuru ambamo viwanda vya magari nchini Marekani vinahitaji mabilioni ya Dola za ziada kutoka serikali, imeleta hali ya wasi wasi.

default

Mwenyekiti wa kampuni la General Motors na mwenyekiti mtendaji Rick Wagoner akizungumzia kuhusu mipango ya kampuni hilo ya mageuzi katika mkutano na waandishi habari mjini Detroit siku ya Jumanne.

Mipango mipya ya kujinusuru ambamo viwanda vya magari nchini Marekani vinahitaji mabilioni ya Dola za ziada kutoka serikalini , imeleta hali ya wasi wasi , wakati hofu kubwa juu ya ukuaji wa uchumi wa dunia imesababisha masoko ya hisa kuporomoka jana Jumatano.

Katika hatua hizo za kujinusuru kampuni kubwa kabisa la kuunda magari nchini Marekani , General Motors , linapanga kupunguza nafasi 26,000 za kazi nchini humo. Kutokana na hali hiyo wafanyakazi wa kiwanda cha magari cha Opel nchini Ujerumani ambacho ni kiwanda tanzu cha General Motors , nafasi zao za kazi zimeingia mashakani pia.


Kampuni ya General Motors na Chrysler LLC zimejitahidi kufikisha muda uliopangwa wa kutoa maelezo kuhusu mipango yao ifikapo siku ya Jumanne, siku ambayo rais Barack Obama alitia saini kuwa sheria mpango wa dola bilioni 787 wa matumizi na punguzo la kodi wenye lengo la kuchochea uchumi wa taifa hilo lenye uchumi mkubwa kabisa duniani.

Ni mpango mkubwa kabisa wa aina yake wa kichocheo cha uchumi katika historia ya Marekani, lakini wawekezaji wameachwa wakiwa midomo wazi kuwa, kama rais Obama alivyosema , utakuwa ni alama ya mwanzo wa mwisho wa matatizo ya kiuchumi ya Marekani.

Wawekezaji pia wametia shaka iwapo viwanda vya magari nchini Marekani vitaweza kurejea katika hali ya kupata faida tena bila ya kwanza kupitia hatua ya kurekebisha kufilisika kwao ambayo itakuwa na maana ya kufunga kwanza baadhi ya viwanda na kupoteza mamia kwa maelfu ya nafasi za kazi.

Iwapo hali hiyo itatokea , itakuwa hatua ndefu na ya mkanganyiko ambayo itachafua zaidi imani katika uchumi ambao tangu hapo uko katika hali ya wasi wasi, amesema Michael Sheldon wa taasisi ya fedha katika jimbo la Connectcut.

Hali ya majaaliwa ya kampuni tanzu ya Opel nchini Ujerumani ya General Motors, amesema mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo mjini Detroit Rick Wagoner kuwa bado haijulikani. Inawezekana kiwanda cha Opel nchini Ujerumani kikafungwa ama kampuni hiyo ikauzwa. Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi wa kampuni ya Opel mjini Bochum Rainer Einenkel anasema kuwa hatma ya kiwanda hicho inapaswa kuachiwa wafanyakazi kujua watafanyanini.

Kwa jumla kampuni la General Motors inataka kupunguza nafasi za kazi 47,000. Katika ombi lao kwa serikali ya Marekani kampuni ya GM imetaka kupatiwa kiasi cha dola bilioni 30. Hii ni karibu mara mbili kuliko kampuni hilo la GM lilivyoomba hapo kabla.

Waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westfalia Jürgen Rüttgers, anataka kuweka wazi kabla ya ziara yake nchini Marekani kuwa mpango huo wa kichocheo cha uchumi utakuwa na maana gani kwa kampuni la Opel nchini Marekani.


Sekione Kitojo/RTRE/DPAE

►◄
 • Tarehe 18.02.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GwZP
 • Tarehe 18.02.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GwZP
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com