1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamo wa Rais wa Marekani Dick Cheney kuzuru Mashariki ya Kati

11 Machi 2008

Ikulu ya Marekani imetangaza kwamba Makamo wa Rais wa Marekani Dick Cheney atafanya ziara Mashariki ya Kati hapo Jumapili.

https://p.dw.com/p/DMMY

WASHINGTON

Rais George W. Bush amesema mjini Washington kwamba lengo la Cheney ni kuwahikishia watu kwamba Marekani imejifunga kuleta amani Mashariki ya Kati.

Cheney anatazamiwa kutembelea Israel na Ukingo wa Magharibi lakini anakabiliwa na matatizo mapya.Israel hapo jana imetangaza kwamba inatanuwa makaazi mapya ya walowezi wa Kiyahudi hususan katika eneo la Jerusalem ya Mashariki linalokaliwa kwa kiasi kikubwa na Waarabu.Machafuko ya umwagaji damu karibu na ndani ya Gaza pia yameongezeka katika wiki za hivi karibuni.

Marekani hapo jana imekosowa mpango huo wa Israel kujenga makaazi mapya ya walowezi wa Kiyahudi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mpango huo unakiuka mpango wa ramani ya amani Mashariki ya Kati na sheria ya kimataifa.

Jumuiya ya kimataifa pia imeshutumu mpango huo na kuonya kwamba unaweza kukwamisha juhudi za kuanzisha upya mazungumzo lege lege ya amani.

Katika ziara yake hiyo Makamo wa Rais wa Marekani Cheney pia anatazamiwa kutembelea Uturuki,Oman na Saudi Arabia ambapo anategemewa kuzungumzia wasi wasi wa Marekani juu ya bei za mafuta kutokana na bei ya mafuta ghafi hapo jana kuweka rekodi mpya wakati fulani kwa kufikia dola 108 kwa pipa.