Makamishna wa Tume ya Ulaya waidhinishwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.02.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Makamishna wa Tume ya Ulaya waidhinishwa

Bunge la Ulaya leo limeikubali tume ya Ulaya ilio na makamishna wepya, chini ya uongozi wa mkuu wa tume, Manuel Barroso. Uamuzi huo unamaliza Vuta N'kuvute iliodumu miezi mitatu sasa katika Umoja wa Ulaya.

Jose Manuel Barroso,rais wa Tume ya umoja wa Ulaya, akiwahutubia waandishi wa habari

Jose Manuel Barroso,rais wa Tume ya umoja wa Ulaya, akiwahutubia waandishi wa habari

Wabunge kwa wingi mkubwa- kura 488 zikiunga mkono na 137 zikipinga- walitoa kibali chao kwa makamishna 26 wa tume hiyo watakaosimamia shughuli mbali mbali. Makamishna hao waliteuliwa na serekali za nchi zao, wanachama wa Umoja wa Ulaya. Kulikuweko wabunge 72 waliojizuwia kupigia kura upande wowote, hawajawakubali au kuwakataa makamishna hao.

Mkuu wa tume ya Ulaya, Manuel Barroso, ambaye anaanza kazi kwa awamu ya pili, alisema baada ya uamuzi huo, na hapa ninamnukuu: kutokana na uhalali wa kidemokrasia tulioupata kutoka kwenu, tuna fahari na imani kufanya kazi kwa nia kamili kwa ajili ya maslaha ya demokrasia ndani ya Ulaya, Ulaya ambayo ni tochi ya uhuru duniani.

Matokeo hayo ya kura hayajamstaajabisha mtu yeyote baada ya mwezi uliopita bunge hilo la Ulaya lilipolazimisha ajiuzulu mtetezi wa ukamishna aliotokea Bulgaria na ambaye alipangiwa ashughulikie masuala ya misaada ya kiutu. Lakini bunge hilo liliwaunga mkono watetezi wengine. Hiyo ndio sababu ya kuchelewa kuidhinishwa tume hii mpya, na Manuel Barroso alibakia kama mkuu wa kujishikiza wa chombo hicho cha Umoja wa Ulaya. Kabla ya kupigwa kura Barroso alitoa mwito kuweko uwiano wa karibu zaidi baina ya nchi 27 wanachama kuhakikisha uchumi wa nchi zao unapanda. Alisema ushirikiano mkubwa zaidi baina ya nchi hizo utaupa Umoja wa Ulaya sauti yenye nguvu zaidi duniani. Alisema Ulaya inahesabika pale nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanapozungumza kwa sauti moja ilio na nguvu, na pale maslahi ya Ulaya yanapofafanuliwa wazi wazi na kutetewa vilivyo, hasa katika masuala ya biashara na siasa za ushindani. Manuel Barroso alisema Ulaya inapata mafanikio machache pale nchi wanachama zinapozungumza kwa kila nchi kujipigania maslahi yake yenyewe yalio finyu, tena kwa njia isiokuwa na uwiano baina ya nchi wanachama. Alitoa mfano wa karibuni wa Haiti ambapo Umoja wa Ulaya umefanikiwa kwa kuchukuwa hatua kwa pamoja.

Kura ya mara hii ya kuliunga mkono baraza zima la makamishna linafungua njia kwa tume mpya ya Umoja wa Ulaya kuanza kufanya kazi kwa miaka mitano ijayo, japokuwa inabidi ipewe kibali cha mwisho na nchi zote 27 zilizo wanachama wa Umoja wa Ulaya. Tume ya Ulaya, japokuwa haichaguliwi moja kwa moja na wananchi, inapendekeza sheria mpya na inasimamia mikataba ya Umoja wa Ulaya. Pia inasimamia masuala ya ushindani wa kibiashara miongoni mwa nchi wanachama na inasimamia zoezi la kuupanua Umoja wa Ulaya kwa kuziingiza nchi nyingine za Ulaya kama wanachama wepya.

Jopo jipya la makamishna, ndani yake akiwemo mkuu mpya wa masuala ya kigeni, Catherine Ashton, linapanga kuwa na mkutano wake kamili Februari 17.

Ni tu vyama vya kijani, wakoministi na makundi ambayo yana wasiwasi na fikra ya Muungano wa Ulaya nadani ya bunge ndio yaliowapinga makamishna wepya. Mbunge wa chama cha Kijani cha Ujerumani Reinhard Bütikofer, alisema:

" Kundi langu haliiunga mkono tume hii. Sisi haturidhika na orodha ya watu wanaokamata nyadhifa. Kwanza sisi tulitaka kwamba nchi wanachama zinazoteuwa makamishna zingeteua wanawake wengi zaidi. Sasa ni thuluthi moja. Pia sisi tunahisi kwamba Rais wa Tume, Bwana Barroso wa kutoka Ureno, ambaye kwa sehemu nyadhifa hizo amezikata, amepanda mzizi wa kuweko mabishano baina ya makamishna."

Suala muhimu la tume mpya litakuwa juu ya namna ya kusaidia kuipiga jeki juhudi za nchi za Ulaya kujikwamua na hali ya uchumi wa nchi hizo kwenda chini wakati ambapo kuna nakisi kubwa za bajeti huko Ugiriki, Spain, Ureno na nchi nyingine, hali ambayo inazusha wasiwasi katika eneo la nchi zenye kutumia sarafu ya Euro na pia nje ya eneo hilo.

Kuna kamishna moja kutoka kila nchi 27 wanachama,Lakini wote wanatakiwa kufanya kazi kwa maslahi ya Umoja wa Ulaya, kwa ujumla.

Mwandishi: MIraji Othman/ AFP/dpa/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdulrahman