Makaazi ya Naibu Rais wa Kenya yashambuliwa | Matukio ya Afrika | DW | 29.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Makaazi ya Naibu Rais wa Kenya yashambuliwa

Watu wenye silaha ambao hawakutambuliwa wameshambulia nyumbani kwa Naibu Rais wa Kenya William Ruto siku ya Jumamosi, zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kuelekea uchaguzi mkuu nchini humo.

Ruto hakuwa nyumbani wakati wa shambulizi hilo lililomsababishia majeraha makubwa mmoja wa askari wa kitengo maalumu cha polisi (GSU), alisema afisa usalama ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa hakuwa na idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari.

"Kuna watu wenye silaha waliopanga mashambulizi hayo na wamempiga risasi ofisa wa GSU na kuiba silaha yake," alisema afisa huyo.

Idara za usalama zinajaribu kubaini iwapo kulikuwepo na washambuliaji wengine katika makaazi makubwa ya naibu wa rais huyo yalioko karibu na mji wa Eldoret, umbali wa kilomita 312 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Kenya Nairobi, alisema afisa mwandamizi.

Askari zaidi wamepelekwa na operesheni ya usalama inaendelea, alisema afisa huyo. Ruto ndiye mgombea mwenza wa rais Uhuru Kenyatta, ambaye anakabiliwa na mchuano mkali wa kuchaguliwa tena Agosti 8, dhidi ya kiongozi wa upinzani wa muda mrefu Raila Odinga.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Lilian Mtono