1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi yamiminika Mali

Admin.WagnerD17 Januari 2013

Nchi mwanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi kwa Nchi za Afrika ya Magharibi, ECOWAS, zimetangaza kuingia katika mapambano ya kuwang'oa waasi kaskazini mwa Mali.

https://p.dw.com/p/17LXN
Malian National guards patrol on January 16, 2013 at a military airbase in Bamako as president Dioncounda Traore visit French troops. French troops battled Islamist rebels in Mali today in a war which escalated as Al Qaeda-linked fighters claimed to have taken 41 foreigners hostage in a retaliatory attack in neighbouring Algeria. AFP PHOTO / ISSOUF SANOGO (Photo credit should read ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images)
Mali Nationalgarde Airbase in Bamako 16. Januar 2013Picha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Azimio hilo linafikiwa wakati huu ambapo Umoja wa Ulaya uko mbioni kuupitisha mpango wa kupeleka wakufunzi wa kijeshi kuvinoa vikosi vya Mali.

Mwakilishi maalumu wa mwenyekiti wa ECOWAS, Aboudou Toure Cheaka, amesema kuwa Nigeria iko tayari kupeleka vikosi vyake nchini Mali ili kusaidia mapambano dhidi ya waasi.

Vikosi hivyo vinatarajiwa kutua nchini Mali katika kipindi cha takriban wiki moja baada ya vikosi vya Ufaransa kuanza operesheni ya kuiokoa Mali kutoka mikononi mwa makundi ya waislamu wenye itikadi kali.

Bwana Cheaka amesema pia kuwa vikosi vingine kutoka Algeria vitapelekwa hii leo katika eneo la mpaka baina ya nchi hiyo na Mali. Pamoja na hivyo, Togo na Burkina Faso nazo zitapeleka wanajeshi wake nchini Mali mwishoni mwa juma hili au mwanzoni mwa juma lijalo. 

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: dapd

Vikosi hivyo vinatumwa kuongeza nguvu ya vile vya Ufaransa vinavyowajumuisha wanajeshi 800 ambavyo tayari viko Mali vikipambana na makundi ya waasi. Ufaransa imeahidi kuongeza wanajeshi wake nchini humo na kufikia 2,500 pamoja na vifaa kama vile helikopta za kijeshi, ndege za kivita, ndege za kijeshi za kufanyia uchunguzi kubaini walipo waasi pamoja na vifaru.

Umoja wa Ulaya kusaidia mafunzo ya kijeshi

Mapambano ya kuwatoa waasi nchini Mali yanazidi kupata uungaji mkono wa kimataifa ambapo hii leo mjini Brussels Ubelgiji, Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana kuupitisha mpango wa kupelekwa wakufunzi wa kijeshi kwa ajili ya kuvinoa vikosi vya Mali. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Mali, Tieman Coulibaly, naye anashiriki kikao cha leo mjini Brussels.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye nchi yake inashiriki pia katika kikao cha Brussels alisema kuwa kuna haja ya kuisaidia Mali katika mzozo ilionao.

"Naamini kuwa tuko katika shinikizo la wakati. Ujerumani inaona kuwa usalama wa eneo la magharibi ya Afrika ni sawa na Usalama wake.  Bila shaka ugaidi uliopo kaskazini mwa Mali si kitisho kwa Afrika tu bali pia kwa Ulaya" alisema Merkel.

Burkina's President Mwenyekiti wa ECOWAS Rais Alassane Ouattara katika moja ya vikao vya jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa ECOWAS Rais Alassane Ouattara katika moja ya vikao vya jumuiya hiyo.Picha: PIUS UTOMI EKPEI/AFP/Getty Images

Afisa wa ngazi za juu katika umoja huo amesema kuwa suala la kupeleka wakufunzi hao sasa limekuwa ni la lazima na linatakiwa litimizwe haraka iwezekanavyo na kwamba wanaangalia pia uwezekano wa kupeleka misaada mingine inayohitajika.

Hata hivyo taarifa kutoka umoja huo zinasema kuwa wakufunzi hao hawataanza kazi mara moja hadi hapo hali itakaporejea katika utulivu kwenye eneo la kusini mwa Mali ambapo ndipo vitakapoweka kambi. Vikosi kamili vya mafunzo vinatarajiwa kuingia Mali mwezi Februari mwaka huu.

Umoja wa Ulaya pia unatarajia kuishinikiza serikali ya mpito ya Mali kuufanyia kazi mpango wa kuwa na serikali kamili ili iweze kupata fedha za msaada.

Baadhi ya Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya wakiwa Brussel
Baadhi ya Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya wakiwa BrüsselPicha: REUTERS

Kwa upande wake Marekani imesema kuwa inaangalia ni aina gani ya msaada iipe Ufaransa ambayo inapambana na waasi  nchini Mali. Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Leon Panetta, amesema kuwa nchi yake haina mpango wa kupeleka vikosi Mali. 

Mwandishi: Stumai George/Dpa/Ape/Reuters

Mhariri: Josephat Charo