Majeshi ya nchi kavu ya Israel yashambulia huko Gaza | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Majeshi ya nchi kavu ya Israel yashambulia huko Gaza

Wanajeshi wa nchi kavu wa Israel wazidi kuingia Ukanda wa Gaza

default

Mpalestina anambeba mwanawe aliyejeruhiwa baada ya kufanywa shambulio la roketi la Israel huko Beit Lahiya, kaskazini ya Gaza

Kile kitisho kilichotolewa na Israel kwa masiku kwamba itapeleka wanajeshi wake wa nchi kavu huko Gaza sasa kimetimia, tangu jumamosi iliopita. Wanajeshi wa nchi kavu na vifaru wameingia katika maeneo ya Wapalastina, licha ya pia kuendeshwa mashambulio kutoka angani na baharini. Zaidi kuhusu mashambulio yanayoendeshwa na jeshi la Israel huko Gaza, yasikilize maoni yalioandikwa na Peter Philipp wa hapa Deutsche Welle.

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, na wasemaji wengine wa nchi hiyo, wamehakikisha kwamba mashambulio yanayofanywa na wanajeshi wa nchi kavu wa nchi hiyo huko Gaza hayakusudii kuumaliza utawala wa Chama cha Hamas katika Ukanda huo, lakini ni kufanya tu isiwezekane kwa Israel kushambuliwa na maroketi yanayofyetuliwa kutokeaa ukanda huo.

Lakini ukweli wa mambo huko ni mwengine, licha ya kwamba waandishi wa habari wa kimataifa hawaruhusiwi na Israel kuingia katika ukanda huo. Mashambulio yaliofanywa na Israel yamewalenga wawakilishi wakuu wa chama cha Hamas, yameyaharibu majengo ya wizara na ya taasisi za utawala, na bila shaka, matokeo ni kuendelea kuuliwa na kujeruhiwa raia. Katika kila watu wanne waliokufa mmoja ni raia. Hayo yote hayahusiani na kuyanyamazisha mashambulio ya maroketi, lakini zaidi kukinyamazisha Chama cha Hamas.

Japokuwa malengo hayo yote mawili hayawezi kufikiwa kwa kutumia mabomu mnamo muda mfupi au wa wastani ujao, lakini jumamosi iliopita majeshi ya nchi kavu yameingia vitani. Na japokuwa kwa masiku kadhaa watu waliyaona majeshi hayo yakikusanywa katika mpaka na Ukanda wa Gaza, hata hivyo, watu walishtuka pale yalipopewa amri ya kujiingiza Gaza na kushambulia. Kuingia kwao Gaza kumeyapa sura mpya malumbano haya ambayo matokeo yake hayajulikani zaidi kuliko ilivokuweko hapo kabla.

Mashambulio ya angani yanaweza kusitishwa fumba na kufumbua, lakini sio hujuma za nchi kavu. Pia kuyaondosha majeshi hakutakiwi kuonekana kwa macho ya wale walio na dhamana kuwa ni kushindwa au kwamba wanakimbia kushindwa, ama sivyo wale wote walioathirika na vita hivyo, hata wa upande wa watu waliovianzisha, wataviona vita hivyo kuwa visivokuwa na maana. Hivyo, kuondoa au kurejesha nyuma majeshi lazima kufungamanishwe na mafanikio. Sasa, tujiulize: mafanikio gani ambayo Israel inatarajia kuypata huko Gaza?

Kinachotakiwa sio tu uhakika kwamba itafika siku ambapo hakuna maroketi tena yatakayofyetuliwa kutoka Gaza kwendea Israel; lakini zaidi ni kwamba nguvu za Chama cha Hamas katika Ukanda wa gaza zinavunjwa, kwamba Chama cha Fatah cha Rais wa Wapalastina, Mahmoud Abbas, kirejee madarakani huko Gaza, hivyo baadae Israel iwe na mshirika anayekubalika wa kuzungumza nayo.

Yaweza kwamba hili ni jambo lililo mbali kufikiwa, lakini mwishowe hizo ndizo hesabu inazozipanga serekali ya Ehud Olmert, japokuwa kuna ushahidi wa kutosha kuonesha kwamba serekali hiyo hiyo ya Israel haijamtilia maanani sana huyo mshirika wa mazungumzo inayomkubali. Mbadala pekee mwengine ni kuuteka upya Ukanda wa Gaza kwa muda; lakini jambo hilo halitakiwi na mtu yeyote huko Israel.

Hivyo, inafikiriwa kujiingiza kijeshi huko Gaza hakutaleta ufumbuzi kwa masuali na matatizo yalioko, na mwishowe huenda tukawa tena na usitishaji wa mapigano wenye kulegalega, hivyo kupangwa tangu mwanzo kuweko duru ijayo ya mapigano. Mamia ya watu ziyada watakaokufa wataitia sumu zaidi hali ya mambo na mapambano hayo kila wakati yatakuwa makali zaidi.

Kila mtu yafaa aitafakari hali hii, hasa wale walioko huko Marekani, lakini na pia wale watu walioko katika miji mikuu ya nchi za Ulaya, mji wa Berlin ukiwemo, ambao wanalifahamu vibaya suala la kuwa na mashikamno na Israel.Hao ni watu wanaozuwia kutolewa miito ya kusitishwa mapigano, kwa vile Israel ina haki ya kujilinda yenyewe. Bila ya shaka, Israel inayo haki hiyo. Lakini kwa vile yaonekana nchi hiyo inazidi kuiingia katika michafuko, polepole ingekuwa uzuri ijilinde yenyewe.

 • Tarehe 05.01.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GSLU
 • Tarehe 05.01.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GSLU
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com