1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Marekani yaanza kuondoka kaskazini mwa Syria

Grace Kabogo
7 Oktoba 2019

Vikosi vya Kikurdi vinavyoungwa mkono na Marekani nchini Syria vimesema majeshi ya Marekani yameanza kuondoka kwenye maeneo ya mpaka wa Syria na Uturuki.

https://p.dw.com/p/3QolX
Syrien Raʾs al-ʿAin | Syrische Kurden und US Militärfahrzeug nahe der Grenze zur Türkei
Picha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Hatua hiyo imechukuliwa saa chache baada ya Ikulu ya Marekani kutangaza kwamba vikosi vyake havitaunga mkono operesheni ya Uturuki katika eneo la kaskazini mashariki mwa Syria.

Wanamgambo wa vikosi vya Kikurdi vinavyopigania demokrasia nchini Syria, SDF, wamesema kuwa majeshi ya Marekani yanaondoka wakati ambapo Uturuki inajiandaa kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na Wakurdi kaskazini mashariki mwa Syria.

Taarifa ya kundi la SDF imeonya kuwa uvamizi wa Uturuki kwenye eneo hilo litakuwa ni pigo katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Majeshi ya Marekani yaondoka Ras al-Ayn na Tal Abyad

Shirika la habari la vikosi hivyo, Hawar pamoja na shirika la kufatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza pia vimeeleza kwamba  majeshi ya Marekani yameanza kuondoka siku ya Jumatatu kwenye maeneo karibu na miji ya Ras al-Ayn na Tal Abyad.

Jana usiku Ikulu ya Marekani ilitangaza kuwa nchi hiyo itayaondoa majeshi yake kaskazini mashariki mwa Syria na haitounga mkono operesheni ya anga na ardhini iliyopangwa na Uturuki. Matamshi hayo yametolewa muda mfupi baada ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kutangaza kwamba Uturuki itaanzisha operesheni ya kijeshi.

USA trump und Erdogan Treffen in New York
Rais Erdogan akiwa na Rais TrumpPicha: Reuters/K. Lemarque

Aidha, taarifa ya Ikulu ya Marekani pia ilizikosoa Ufaransa, Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya kwa kushindwa kuwarudisha nyumbani raia wake waliojiunga na IS, ambao wanashikiliwa nchini Syria

Jana Erdogan alizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump ambapo walijadiliana kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa eneo salama mashariki mwa Mto Euphrates. Erdogan alirudia kusisitiza msimamo wake wa kuanzishwa ''eneo salama'' hatua itakayotuliza kitisho kinacholetwa na Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi, PKK na kundi la wanamgambo wa Kikurdi, YPG linaoungwa mkono na Marekani.

Erdogan asikitishwa kutotekelezwa makubaliano

Erdogan alisema hatua hiyo itasaidia kuanzisha mazingira muhimu ya kurejea kwa wakimbizi wa Syria, ingawa alimueleza Trump masikitiko yake kutokana na majeshi ya Marekani na urasimu wa usalama kushindwa kutekeleza makubaliano kati ya nchi hizo mbili.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu amesema nchi yake imejizatiti kuwaondoa magaidi walioko katika mpaka wake na Syria ambao unadhibitiwa na wanamgambo na amehakikisha kuhusu usalama wa nchi hiyo.

Cavusoglu ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba tangu kuanza kwa mzozo wa Syria wameiunga mkono uadilifu wa nchi hiyo na wataendelea kufanya hivyo kuanzia sasa. Amesema Uturuki itachangia katika amani na utulivu wa Syria.

(AP, AFP, Reuters)