Majeshi ya Afghanistan yaudhibiti mji mkuu | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Majeshi ya Afghanistan yaudhibiti mji mkuu

Afghanistan imeeleza kwamba majeshi yake yamefanikiwa kuudhibiti tena mji wa Kabul uliokuwa umeshambuliwa na waasi wa kundi la Taliban. Shambulizi hilo lilikuwa kubwa zaidi kutokea Kabul katika kipindi cha miaka 10.

Askari wa NATO nchini Afghanistan

Askari wa NATO nchini Afghanistan

Vikosi vya serikali ya Afghanistan ndivyo vilivyoongoza operesheni hiyo ya kuurudisha mji huo mkuu mikononi mwake, lakini msemaji wa jeshi la Jumuiya ya Kujihami ya NATO, amesema kwamba walitoa msaada kwa vikosi hivyo baada ya kuombwa kufanya hivyo. Watu 47 waliuwawa nchini Afghanistan katika mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa kundi lenye msimamo mkali wa Kiislamu, Taliban. Mashambulizi hayo yalifanyika katika mji mkuu Kabul na miji mingine mitatu kwa muda wa masaa 18.

Waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan, Bismillah Mohammadi

Waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan, Bismillah Mohammadi

Katika mkutano na waandishi wa habari, waziri wa mambo ya ndani wa Afghanistan, Bismillah Mohammadi alieleza kwamba mbali na kusababisha vifo vya watu 47, shambulizi la wataliban liliwajeruhi pia watu 65, 40 kati yao wakiwa maafisa wa usalama na 25 raia wa kawaida. Mohammadi alisema kwamba waasi 16 ndio waliofanya mauaji mjini Kabul. "Walipokuwa wakiingia mjini walikuwa wamevaa hijabu . Waliweka maua katika gari lao kuashiria kwamba wanakwenda kwenye sherehe," alieleza waziri huyo.

NATO yaisifu Afghanistan

Milio ya risasi ilianza kusikika Jumapili mchana katika miji ya Kabul, Jalalabad, Gardez na Logar. Kulitokea pia miripuko lakini baadaye wanajeshi wa Afghanistan walianza kujibu mashambulizi ambapo baadhi ya wapiganaji wa Taliban waliuwawa.

Kamanda wa majeshi ya ISAF, Jenerali John Allen

Kamanda wa majeshi ya ISAF, Jenerali John Allen

Kamanda wa jeshi la ISAF la kundi la kujihami la NATO, Jenerali John Allen, amewapongeza maafisa wa usalama wa Afghanistan kwa jinsi walivyopambana na waasi. "Walikuwa wamejipanga vizuri na kuongozwa vizuri na walitumia juhudi yao kulinda maisha ya raia wenzao," alisema Allen.

Naye mkuu wa polisi wa mji wa Kabul, Jenerali Ayoub Salangi, ameeleza kwamba watu 35 walitekwa na waasi karibu na jengo la Bunge la Afghanistan lakini hata hivyo watu hao baadaye waliweza kuokolewa. Kwa mujibu wa mkuu wa polisi, ni mwanamke mmoja tu aliyejeruhiwa.

Ubalozi wa Ujerumani washambuliwa

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amelaani mapigano yaliyotokea Afghanistan na kuahidi kwamba nchi yake itaendelea kuyaunga mkono maendeleo yanayofanyika Afghanistan. "Tutaendelea kupambana na uasi wa magaidi," alisema Westerwelle. Tutaendelea kusaidia kujenga Afghanistan yenye amani na yenye mazingira mazuri ya kuishi. Licha ya kuwekewa vikwazo,tutaendeleza sera yetu ya kulikabidhi jukumu la usalama wa nchi kwa raia ."

Ubalozi wa Ujerumani ni miongoni mwa majengo yaliyoshambuliwa katika mapigano yaliyoanza jana Jumapili. Hata hivyo Westerwelle ameeleza kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa katika ubalozi huo. Wafanyakazi wote walipelekwa mahali penye usalama.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com