Majaji wakubali dhamana ya Bemba | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Majaji wakubali dhamana ya Bemba

Mahakama ya kimataifa ya ICC leo imeamuru kuachiwa huru kwa masharti makamu wa zamani wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Jean Pierre Bemba, kabla ya kuanza kwa kesi inayomkabili kuhusika na uhalifu wa kivita

Jean Pierre Bemba alikamatwa mjini Brussels Mei mwaka jana kufuatia waranti uliyotolewa na mahakama hiyo ya kimataifa ya uhalifi wa kivita ya mjini The Hague

Mahakama hiyo ilisema katika taarifa yake kwamba kuendelea kuzuiliwa  kwa Jean Pierre Bemba hakuelekei kuwa  jambo la lazima na kwamba hakuna sababu ya kuamini kwamba Bemba atavuruga upelelezi au kuendelea kufanya makosa aliyoshtakiwa.

Bemba anakabiliwa na mashtaka ya kuwaongoza wapiganaji wake kuhusika na mateso, ubakaji na mauaji, walipoingia katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika kati kuanzia Oktoba mwaka 2002 hadi Machi 2003.

Lakini kuachiwa huru kwa Bemba kutategemea ni nchi gani itakuwa tayari kumpokea pamoja na  utekelezaji wa masharti yatakayotolewa.

Hata hivyo mwendesha mashtaka  mkuu wa mahakama hiyo ya The Hague Luis Moreno-Ocampo amewasilisha ombi la kupinga uamuzi uliyotolewa na majaji wanaosikiliza kesi hiyo.

Kitengo cha rufaa katika mahakama hiyo ya The Hague kitasikiliza rufaa hiyo ya Ocampo  Tarehe 24 mwezi huu na kuupitia upya uamuzi uliyotolewa wa Bemba kama ulikuwa sahihi.

Luis Moreno Ovampo amesema majaji wa mahakama hiyo wamethibitisha kuwa Bemba ana afya nzuri ya kuweza kusimama kizambani kujibu mashtaka mazito yanayomkabili, na kuongeza kuwa wahanga na mashahidi wa kesi hiyo wasiwe na wasiwasi juu ya usalama wao kwani mahakama hiyo itaendelea kuwalinda.

Jean Pierre Bemba mwenye umri wa miaka 46 mwezi June aliiomba mahakama hiyo kumwachia huru wakati kesi yake ikisubiriwa kusikilizwa.

Mahakama hiyo iliwaalika wawakilishi wa mataifa ya  Ubelgiji, Ufaransa, Ureno, Italia, Ujerumani na Afrika Kusini, nchi ambazo Bemba aliomba apelekwe, kutokana na kuwa na jamaa ua mali.

Akitolea mfano wakili wake Aime Kilolo  amesema, Bemba ana miliki mali na akaunti za benki nchini Ubelgiji ambako watoto wake wanasoma, na pia alikuwa na maingiliano muhimu ya kijamii na Ufaransa.

Hata hivyo kwa mujibu iliyotolewa muda mfupi uliyopita na mahakama hiyo ya The Hague imesema kuwa nchi hizo zimekataa na nyingine kuwa na wasi wasi na ombi la Bemba kwenda katika nchi hizo katika kipindi hiki cha mpito kuelekea kesi yake.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilimkatalia  Bemba ruhusa ya kurudi nyumbani ikisema atakamatwa na kushtakiwa pindi akirejea.

Jean Pierre Bemba, alikuwa mmoja kati ya makamu wanne wa rais katika serikali ya mpito ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada ya vita vya miaka kadhaa vya wenyewe kwa wenyewe.

Mnamo mwaka 2006 alishindwa na Rais Joseph Kkabila katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita.

Baadaye aliendelea kuwa kiongozi wa upinzani akiongoza chama chake cha MLC, ambapo mwaka jana alilazimika kukimbia baada ya majeshi ya serikali yalipopambana na vikosi vyake kujaribu kuwanyang´anya silaha.Kiasi cha watu 300 waliauawa katika mapigano hayo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman     

 • Tarehe 14.08.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JBRj
 • Tarehe 14.08.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JBRj

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com