1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maisha ya watoto Yemen yazidi kutishiwa

Lilian Mtono
14 Septemba 2018

Shirika la kimataifa la misaada la Save the Children limesema mapigano kati ya vikosi vya Yemen na waasi kuzunguka mji wa Hodeida yamesababisha kufungwa kabisa kwa kivuko kinachounganisha Hodeida na maeneo mengine.

https://p.dw.com/p/34r6V
Jemen Krebs Patienten
Picha: Reuters/K. Abdullah

Shirika la kimataifa la misaada la Save the Children limesema mapigano ya hivi karibuni kati ya vikosi vya serikali ya Yemen vinavyoungwa mkono na muungano wa majeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na waasi wa Kihouthi kuzunguka mji wa Hodeida, yamesababisha kufungwa kabisa kwa kivuko kikuu kinachounganisha mji huo wa bandari na maeneo mengine ya nchi hiyo.

Shirika hilo la misaada ya Save the Children limesema lina wasiwasi kuhusu hali ya watoto wapatao milioni 4.2 walioko nchini Yemen, kutokana na kitisho cha njaa. Tamer Kirolos wa Save tha Children amesema suala la kufunguliwa kwa kivuko hicho muhimu kinachounganisha Hodeida na mji mkuu wa Sanaa ni muhimu kwa kuwa linahusu maisha ya watu.

Mashambulizi ya hivi karibuni yalianza wiki iliyopita kufuatia kushindwa kwa mazungumzo ya amani yaliyotarajiwa kuanza upya mjini Geneva. Mazungumzo hayo kati ya wanamgambo wa Houthi na serikali hata hivyo yalivunjika Jumamosi iliyopita. 

Mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini Yemen, Meritxell Relano aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba zaidi ya watoto milioni 11, ambao ni takriban asilimia 80 ya idadi jumla ya watu nchini humo wenye umri wa chini ya miaka 18, wanakabiliwa na upungufu wa chakula, maradhi, kupotea na kukosekana kwa kiasi kikubwa kwa huduma muhimu za kijamii.

Jemen | Huthi Rebellen
Miongoni mwa wapiganaji wa Houthi wanaopambana na vikosi vya serikali nchini Yemen.Picha: Getty Images/AFP/G. Noman

Afisa huyo ameliambia shirika hilo kwamba, watoto hao ambao wengi miongoni mwao ni wa umri wa miaka chini ya miwili wanaotibiwa katika hospitali ya Sab'een ni miongoni mwa watoto wengi wenye utapiamlo mkali kwenye taifa hilo linalokabiliwa na vita kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Vikosi vya serikali vilidai kusimamisha mapigano ili kztoa fursa ya mazungumzo ya amani.

Mamia kwa maelfu ya maisha ya raia nchini humo yanakabiliwa na kitisho katika mji huo wa Hodeida, ambako familia zinaishi kwa hofu ya mapigano na mashambulizi ya angani, hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinaadamu nchini humo, Lise Grande, amesema kwenya taarifa yake kwamba hali inazidi kuzorota nchini humo katika kipindi cha siku chache zilizopita na watu wamekuwa wakipambana ili kuishi.

Madaktari na watoa huduma za afya katika hospitali mbili zilizopo katika mji wa Hodeida wamesema watu 50 wameuawa katika kipindi cha masaa 24, na saba miongoni mwao wakiwa ni wapiganaji watiifu kwa serikali.

Kulingana na Grande, hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo mashambulizi yanataharibu mashine za kusaga nafaka pamoja na maghala ya kuhifadhia nafaka hizo katika eneo hilo la Hodeida.

Vikosi vya muungano mnamo unaoongozwa na Saudi Arabia siku ya Jumatano vilizidhibiti njia zinazotumiwa na waasi  kwa ajili ya usambazaji katika mji huo, na duru za kijeshi zilisema mapigano yaliendelea hadi jana Alhamisi.

Vikosi vya serikali vinavyounwga mkono na muungano huo wa kijeshi, kabla ya wiki hii vilisema vinasimamisha mapigano katika kile walichosema ni kutoa fursa kwa mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/RTRE.

Mhariri: Gakuba, Daniel