1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahujaji wa Gaza wakwama Misri

31 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CiGu

CAIRO

Maafisa wa serikali ya Misri wamewachukuwa zaidi ya mahujaji 1,000 wa Kipalestina kutoka bandari ya Bahari ya Sham ya Nuweiba na kuwapeleka el-Arish kaskazini mwa Sinai wakati maafisa wa Misri,Israel na Palestina wakizungumzia juu ya kurudi kwao Gaza.

Wengi wa mahujaji hao wamegoma kuondoka kwenye mabasi yao hadi hapo watakapokuwa wamerejeshwa Gaza.Mahujaji hao ni kundi la kwanza kubwa linalorudi kwenye ukanda huo uliotengwa wa Wapalestiana baada ya kukamilisha ibada ya hija ya kila mwaka katika mji mtakatifu wa Mecca nchini Saudi Arabia.

Israel inasisitiza kwamba mahujaji hao lazima wote wapitie ukaguzi wa usalama wa Israel kwa kusema kwamba baadhi yao yumkini wakawa wamechukuwa silaha au fedha kwa ajili ya kundi la wanamgambo wa Kiislam la Hamas ambalo linatawala Ukanda wa Gaza.

Rais Hosni Mubarak wa Misri amesema anataka kuona ufumbuzi wa amani unafikiwa katika suala hilo.