1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahojiano ya mgombea wa upande wa upinzani Martin Fayulu

Oumilkheir Hamidou
21 Novemba 2018

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo Corneille Nangaa amefungua rasmi kampeni za uchaguzi. Mgombea wa upande wa upinzani uliogawika Martin Fayulu anatarajiwa kurejea mjini Kinshasa .

https://p.dw.com/p/38fgv
DR Kongo Martin Fayulu
Picha: Getty Images/AFP/T. Charlier

 Martin Fayulu alichaguliwa Novemba 11 iliyopita mjini Geneva kama mgombea pekee wa upande wa upinzani katika uchaguzi wa rais  wa decemba 23 inayokuja dhidi ya mteule wa chama tawala cha rais anaemaliza mhula wake Joseph Kabila, waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary. Hata hivyo siku moja baadae, vigogo wawili wa siasa za jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe wakajitoa katika makubaliano ya Geneva.

Alipoulizwa maoni yake kuhusu uamuzi wa kujitoa chama cha upinzani cha UDPS na mgombea wao Félix Tshisekledi pamoja pia na mwenyekiti wa chama cha cha Umoja kwaajili ya taifa la Congo-UNC, Martin Fayulu alisema mwanzoni alifikiri ni habari za uwongo. Alikumbusha ahadi walizotoa  walipokuwa wanakwenda Geneva wakajiambia wanahitaji kuwa na mgombea mmoja. Kila mmoja aliahidi kumtambua atakaechaguliwa.

Martin Fayulu anazisuta hoja yeye ni mgeni katika siasa za DRC

Mgombea huyo anaeungwa mkono na vigogo wengine wawili mashuhuri, gavana wa zamani wa Katanga anaeishi uhamishoni Moise Katumbi na kiongozi wa zamani wa wanamgambo Jean Pierre Bemba anatajwa kuwa ni dhaifu kuweza kushindana na wagombea wengine 21 wa kiti cha rais. Mwenyewe Martin Fayula lakini anazisuta hoja hizo na kusema hajui kipi kinawafanya waseme hana nguvu kwasababu anasema ameanza siasa kabla ya wote hao. "Nimeshiriki katika mkutano wa taifa huru na nilishiriki katika mapambano yote ya upande wa upinzani. Nilishirikiana na Tshisekedi, niliongoza mihadhara, maandamano. Hakuna yeyote  aliyeshiriki katika pirika pirika za kisiasa kama mie. Wakongomani wananiita "Mwanajeshi wa wananchi, wananita mlinzi wa hekalu. Kama mie si mzito kwanini wananipa majina yote hayo."

  Nasaha ya kuitika wito wa wakongomani

Martin Fayulu anasema amewasihi wote hao wafikirie upya msimamo wao, na kuheshimu makubaliano ya Geneva ambayo anasema wakongomani wanathamini na wasingetaka kuona yanavunjwa.

Zaidi ya wapiga kura milioni 40 wamesajiliwa kupiga kura uchaguzi wa rais utakapoitishwa decemba 23 inaokuja. Hofu zimechomoza lakini kama uchaguzi huo utaitishwa kama ilivyopangwa. Mbali na mivutano kuhusu mitambo ya kupigia kura, matumizi ya nguvu pia yanatishia kukorofisha zoezi la kupiga kura katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na Beni Kivu ya kaskazini.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/DW/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga