1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa Sudan Kusini waahidi kukomesha vita

8 Novemba 2014

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na kiongozi wa waasi Riek Machar Jumamosi (08.11.2014) wamekubali kukomesha vita vya miezi 11 ambavyo vimeuwa maelfu ya watu na kuwapotezea makaazi wengine milioni 1.8.

https://p.dw.com/p/1DjMC
Riek Machar kiongozi wa waasi(kushoto) na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.
Riek Machar kiongozi wa waasi(kushoto) na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.Picha: Ashraf Shalzy/AFP/Getty Images

Viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo wa Nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika IGAD wametaka serikali ya Sudan Kusini na waasi kusitisha mara moja vita vyao vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 11 sasa venginevyo watakabiliwa na vikwazo na pengine hata kuingiliwa kati kijeshi.

Onyo hilo limetolewa mapema Jumamosi na jumuiya hiyo ya IGAD baada ya mazungumzo ya hivi karibuni kabisa kati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na kiongozi wa waasi Riek Machar kushindwa kuzaa makubaliano kamili ya amani.

IGAD imesema pande zote mbili zimeahidi kukomesha uhasama kabisa,mara moja na bila ya masharti baada ya siku mbili za mazungumzo mjini Addis Ababa na imewapa viongozi hao wawili siku 15 tu kukamilisha makubaliano ya kushirikiana madaraka.

Ukiukaji wa makubaliano

Kiir na Machar walikuwa wamesaini makubaliano ya kusitisha mapigano mwanzoni mwa mwaka huu pamoja na makubaliano mengine kadhaa ya kuoyaongezea muda,lakini makubaliano hayo hayakudumu. Jumuiya ya IGAD imesema ukiukaji mwengine wa makubaliano hayo utakabiliwa na hatua kali.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (kushoto) na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn (katikati) wakati wa mkutano wa kilele Addis Ababa.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (kushoto) na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn (katikati) wakati wa mkutano wa kilele Addis Ababa.Picha: Yohannes G/Eziabhare

Taarifa ya jumuiya hiyo imesema ukiukaji wa usitishaji wa mapigano utakofanywa na upande wowote ule utakabiliwa na hatua ya pamoja itakayochukuliwa na jumuiya hiyo ya kanda ikijumuisha kuzuiliwa kwa mali,marufuku za safari na vikwazo vya silaha.

Taarifa hiyo imeongeza kusema kwamba jumuiya ya IGAD bila ya kuzungumza zaidi na pande hizo zinazohasimiana itachukuwa hatua zinazohitajika kuingilia kati moja kwa moja nchini Sudan Kusini kulinda maisha ya raia na kurudisha amani.

Chanzo cha vita

Vita viliripuka nchini Sudan Kusini hapo mwezi wa Disemba mwaka jana wakati Kiir alipomshutumu makamu wake Machar kwa kujaribu kufanya mapinduzi na umwagaji damu ukaanza kuzagaa na kugeuka kuwa mzozo wa kikabila na hivi sasa unajumuisha zaidi ya makundi ya wapiganaji 20.

Jeshi la wananchi wa Sudan SPLA..
Jeshi la wananchi wa Sudan SPLA..Picha: AFP/Getty Images

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limeonya wiki hii juu ya uwezekano wa kuwekwa vikwazo kutokana na mapigano hayo.

Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vimeuwa maelfu ya watu na kuwapotezea makaazi wengine takriban milioni mbili na kuiweka nchi hiyo kwenye ukingo wa baa la njaa huku pande zote mbili zikijihusisha na ukatili uliozagaa kila mahala.

Viongozi wa kanda wamekuwa wakipoteza subira na pande hizo zinazopingana kutokana na kuzorota kwa mazungumzo yao na kuwepo kwa ukiukaji wa usitishaji mapigano mara kwa mara na kabla ya mkutano huu wa karibuni Kiir na Machar walitakiwa wazi wazi "warudishe fahamu zao".

Kujihami tu

Mapigano yamezuka upya katika wiki za hivi karibuni kutokana na kumalizika kwa msimu wa mvua na kumekuwepo na mapigano makali katika maeneo kadhaa hususan karibu na eneo la kuzalisha mafuta la Bentiu.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo Rais Kiir ameahidi kwamba vikosi vyake vitachukuwa hatua katika kujihami tu juu ya kwamba jambo hili limekuwa likitumiwa kama kisingizio na pande zote mbili wakati wa kukiuka suluhu huko nyuma.

Mkutano wa Kilele kuhusu Sudan Kusini mjini Addis Ababa.
Mkutano wa Kilele kuhusu Sudan Kusini mjini Addis Ababa.Picha: Yohannes G/Eziabhare

Amesema "Kuanzia wakati huu hawatoonekana nje ya kambi zao ili kufanya mashambulizi kutoka upande wowote ule.Watapigana tu kwa ajili ya kujihami."

Kiir ameongeza kusema kwamba hicho ndicho anachotaka kuwaambia wananchi wake na kutaka kujitolea kwake upya mbele ya viongozi wa IGAD kwamba chochote wanachokisema hapo watakitekeleza bila ya kushindwa.

Matumaini ya amani

Machar pia amesema amewaamuru wapiganaji wote waasi kusitisha uhasama na kubakia kwenye maeneo yao na kuchukuwa hatua kwa ajili tu ya kujihami.

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar (katikati).
Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar (katikati).Picha: AFP/Getty Images

Amesema "Hatutaki askari yeyote yule auwawe badaa ya mchakato huo wa Addis Ababa na kuongeza kusema kwamba ana imani watafikia makubaliano ya mwisho katika kipindi cha siku 15 waliochoekewa muda wa mwisho.

Wajumbe wanasema serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa itambakisha Kiir katika wadhifa wa urais na kumfanya Machar kuwa waziri mkuu lakini atakuwa na madaraka makubwa kiasi gani limebaki kuwa suala la mvutano.

IGAD jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika inajumuisha Djibouti,Ethiopia,Kenya,Somalia, Sudan Kusini,Sudan na Uganda. Jumuiya hiyo imekuwa ikijaribu kuleta amani nchini Sudan Kusini tokea mwezi wa Januari.

Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka serikali ya Sudan yenye makao yake Khartoum hapo mwaka 2011 na ni taifa changa kabisa duniani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri: Caro Robi