1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama za kiislamu zasogea nyuma Baidoa

Thelma Mwadzaya26 Desemba 2006

Nchini Somalia wapiganaji wa mahakama za Kiislamu wameripotiwa kusogea nyuma baada ya kushambuliwa vikali na majeshi ya nchi jirani ya Ethiopia.

https://p.dw.com/p/CBHp
Wapiganaji wa mahakama za kiislamu mjini Baidoa
Wapiganaji wa mahakama za kiislamu mjini BaidoaPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya muda ya Somalia inatoa wito kwa mahakama hizo kujisalimisha na kuahidi kuwa hawatateswa kwasababu ya imani zao.Mapigano makali kati ya serikali na mahakama hizo yalianza juma moja lililopita baada ya muda wa mwisho wa kuondoka kwa majeshi ya Ethiopia yanayoungwa mkono na serikali kupita.

Mahakama hizo za kiislamu ziliondoa wapiganaji wake katika maeneo ya Dinsoor na Burhakaba ,kusini na mashariki mwa makao makuu ya serikali mjini Baidoa vilevile maeneo ya kati ya nchi.

Siku moja baada ya ndege za vita za Ethiopia kushambulia viwanja vya ndege mjini Mogadishu wapiganaji wa mahakama za kiislamu wameripotiwa kuyakimbia maeneo yaliyo mstari wa mbele karibu na mji wa Baidoa.Viwanja hivyo vya ndege vianmilikiwa na mahakama za kiislamu huku majeshi hayo yanayoungwa mkono na serikali yakipambana nao.

Wakati huohuo msemaji wa serikali ya Somalia Abdirahman Dinari anatoa wito kwa maelfu ya wapiganaji wa kigeni wanaoaminika kuunga mkono mahakama hizo za kiislamu kuondoka ili Wasomali waweze kutafuta suluhu wenyewe.Nchi ya Somalia imezongwa na vita tangu mwaka 91 wakati rais Mohammed Siad Barre alipongolewa madarakani.

Baada ya Rais Siad Barre kufurushwa madarakani mwaka 91 wababe wa kivita walijinyakulia sehemu kwa sehemu.Kulingana na serikali majeshi yake yakishirikiana na yale ya Ethiopia yalishambulia maeneo yanayomilikiwa na mahakama za kiislamu jambo lililoungwa mkono na wakazi wa eneo hilo.

Mahakama za kiislamu zimekuwa zikipata nguvu tangu mwezi Juni huku zikitishia madaraka ya serikali ya muda inayotambulika kimataifa.Serikali hiyo inaungwa mkono na majeshi ya Ethiopia jambo ambalo mahakama hizo zinasema kuwa zinahatarisha usalama wa nchi.

Nchi ya Ethiopia inashikilia kuwa itaendelea kushambulia maeneo maalum nchini Somalia huku wapiganaji wa mahakama za kiislamu wakiendelea kuyaondoka maeneo ya mbele yaliyoshambulia na majeshi ya Ethiopia.Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mawasiliano.