1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yaruhusu taarifa za kifedha za Rais Trump kutolewa

Saumu Mwasimba
10 Julai 2020

Mahakama ya juu Marekani imepitisha uamuzi kwamba mwendesha mashtaka mkuu wa jiji la NewYork ana haki ya kupata taarifa za masuala ya kifedha za Rais Donald Trump ikiwemo taarifa za ulipaji wake wa kodi.

https://p.dw.com/p/3f65E
USA Washington | Oberster Gerichtshof fordert die Übereichung Trumps Steuerklärung
Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Hata hivyo mahakama hiyo imelizuia bunge kupata taarifa kama hizo.

Mahakama kuu ya Marekani kwenye uamuzi wake huo uliotolewa jana Alhamisi imelizuia bunge kupata nyaraka zenye taarifa sawa na hizo kwa sasa. Maamuzi hayo yalifanyika kwa pamoja na kwa hivyo sasa inamaanisha nyaraka muhimu za taarifa za Trump kuhusu masuala yake ya kifedha kwa sasa zitaendelea kuwekwa siri na hazitotolewa kwa umma.

Kesi hii iliyowasilishwa na bunge ilikuwa ikimuweka rais huyo wa Marekani katika nafasi ya kumulikwa zaidi kisiasa na hasa katika kipindi hiki ambapo uchaguzi unakaribia. Uchaguzi mkuu nchini Marekani utafanyika miezi minne kutoka sasa.

Mwendesha mashtaka wa Manhattan: Ni uamuzi wa kihistoria

Hata hivyo ni pigo kwa Rais Trump katika kesi hii ya mwendesha mashitaka wa Manhattan ya kutaka jopo la Mahakama liyaite mahakamani makampuni ya mahesabu ya rais huyo ambapo jopo hilo liliamua kuzipinga hoja za Rais Trump kuhusu kuwa na kinga maalum kama rais. Mwanasheria huyo ameutaja uamuzi wa mahakama kuwa ushindi wa kihistoria wa mfumo wa mahakama nchini Marekani.

Uamuzi uliotolewa sasa unaweza kufungua njia kwa mwanasheria huyo wa jiji la New York kuzipata rikodi za masuala ya fedha ya rais Trump ingawa bado mivutano zaidi ya kisheria inasubiri kuendelea kushuhudiwa.

Juhudi za Rais Trump kupinga wito huo ziliambulia patupu
Juhudi za Rais Trump kupinga wito huo ziliambulia patupuPicha: Getty Images/AFP/J. Watson

Katika maoni yaliyoungwa mkono na upande mkubwa wa jopo la mahakama, mwanasheria mkuu John Roberts aliandika hakuna raia yoyote, hata rais aliyeko juu ya sheria na wajibu wa kutoa ushahidi anapotakiwa kufanya hivyo katika mchakato wa kuchunguza uhalifu.

Juhudi za Trump kupinga hatua hiyo zaambulia patupu

Mahakama hiyo ya juu ya Marekani haikutowa moja kwa moja amri ya kutaka nyaraka hizo ziwasilishwe mahakamani na kwa hivyo uamuzi uliotoka umeonesha kwamba rais Trump huenda akajaribu kupambana kupinga kuitwa mahakamani kama mtu yoyote, kwa misingi ya kisheria kutokana na kutotolewa kwa ombi hilo.

Mwanasheria wa Trump amesema timu yao ya kisheria itaendelea kuzipinga kesi zote mbili za kutaka rekodi za masuala ya kifedha ya rais Trump yawekwe wazi katika mahakama za chini.

Jay Sekulow amesema kwamba wameridhishwa na uamuzi wa mahakama kuu kwa sababu umezuia kwa muda kesi zote mbili ya Bunge na ile ya waendesha mashtaka wa jiji la New York ya kutaka kupata taarifa za masuala ya kifedha za rais Trump.

Kadhalika katika ujumbe wa Twitta mwanasheria huyo wa Trump ameandika kwamba sasa watakachofanya ni kuyaibua masuala zaidi ya kikatiba na kisheria katika mahakama ya chini kuzipinga kesi hizo.