Mahakama Uganda yaamuru Bobi Wine aachiliwe mara moja | Matukio ya Afrika | DW | 25.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mahakama Uganda yaamuru Bobi Wine aachiliwe mara moja

Mahakama Kuu nchini Uganda Jumatatu imeviamuru vikosi vya usalama kukomesha mara moja kuizingira nyumba ya mgombea urais Bobi Wine. Bobi Wine amekuwa chini ya mzingiro tangu alipomaliza kupiga kura yake Januari 14.

Wanajeshi waliojihami kwa silaha nzito na maafisa wa polisi wanaozingira nyumba yake wamewazuwia wanachama wa familia ya Bobi Wine, akiwemo mke wake Barbie, kuondoka nyumbani hapo.

Wiki iliyopita, balozi wa Marekani pia alizuwiwa kumtemebea mwanasiasa huyo na nyota wa muziki, ambaye alishinda asilimia 35 ya kura kwa mujibu wa matokeo rasmi.

Soma pia: Maoni: Ushindi wa Museveni ni wa mashaka

Akiwa katika kitengo cha kesi za kiraia cha Mahakam Kuu mjini Kampala, Jaji Michael Elubu amekubaliana na shauri lililowasilishwa na mawakili wa Wine wakiomba kuachiliwa kwake.

Afrika | Kenia Uganda Proteste Bobi Wine Opposition

Wafuasi wa Bobi Wine wakiwa katika mmoja ya maandamano ya kushikiza kuachiwa kwake.

"Kuendelea kuweka vizuwizi na kumshikilia muombaji nyumbani kwake ni kinyumecha sheria na ukiukaji wa hali yake ya uhuru," alisema Elubu.

"Baada ya kugundua kuwa vizuwizi hivi ni kinyume cha sheria, inaamuriwa hivyo viondolewe."

Serikali ya Uganda ilikuwa imetoa hoja kwamba vizuwizi hivyo dhidi ya mienendo ya Bobi Wine vilikuwa hatua za kinga kwa ajili ya ulinzhi wake mwenyewe na kuzuwia maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi, ambayo Wine anasema yalifanyiwa udanganyifu kumpendelea rais Yoweri Museveni.

Soma pia: Umoja wa Ulaya wakosoa ukandamizaji wa upinzani Uganda

Vikosi vya usalama vilikuwa bado havijaondoka katika eneo linalozunguka nyumba ya Wine, kulingana na msaidizi wake Abdu Hakim.

Vikosi vya usalama nchini Uganda vimekuwa vikipuuza amri za mahakama katika siku za nyuma kuwaachia watu, au vimewakamata tena mara moja watu walioachiwa na mahakama.