Magufuli amtosa Makamba, ambeba Bashe | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Tanzania

Magufuli amtosa Makamba, ambeba Bashe

Rais John Magufuli wa Tanzania amefanya mabadiliko mengine madogo kwenye baraza lake la mawaziri, akimuondosha waziri aliyekuwa na dhamana ya mazingira na muungano, January Makamba.

Mabadiliko hayo yaliyotangazwa leo (Julai 21) na Ikulu ya nchi hiyo yanamuweka Makamba kwenye orodha ya wajumbe kadhaa waliotemwa kutoka serikali ya Magufuli ndani ya kipindi cha miaka minne ya utawala wake. 

Nafasi ya Makamba imejazwa na George Simbachwene ambaye pia aliwahi kufukuzwa kwenye baraza la mawaziri la awamu hii. 

Bashe, anayewakilisha jimbo la Nzega bungeni, amepewa unaibu waziri wa kilimo. Kupitia akaunti yake ya Twitter, mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kulalamika bungeni kwamba alitekwa na watu waliojitambulisha kuwa "usalama wa taifa" kwa sababu ya ukosowaji wake kwa utendaji wa serikali, alimshukuru Rais Magufuli kwa kumpa nafasi hiyo. "Ni jukumu zito. Nimelipokea na kwa uwezo wa Allah, tutavuuka."

Akiandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii kuhusu kufukuzwa kwake uwaziri, January Makamba amesema kwamba ameyapokea mabadiliko hayo "kwa moyo mweupe kabisa," akiahidi kwamba katika siku za baadaye atalizungumzia kwa undani suala hili. 

Taarifa ya Ikulu jijini Dar es Salaam haikufafanuwa sababu za mabadiliko hayo, lakini wengi wanayahusisha na msuguano wa ndani ya serikali na chama tawala, kufuatia tamko la makatibu wakuu wawili wastaafu wa chama hicho na baadaye kile kinachotajwa kuwa sauti za mazungumzo ya simu yaliyovujishwa wiki iliyopita. Mmoja wa makatibu hao wastaafu, ni baba yake January Makamba, Mzee Yussuf Makamba.

Mbali na makatibu wakuu hao wastaafu, sauti hizo za mazungumzo ya simu ambazo bado hazijatolewa maelezo na polisi ya nchi hiyo, zinawahusisha pia mbunge wa jimbo la Mtama lililoko kusini mwa Tanzania, Nape Nnauye na waziri katika serikali ya awamu ya nne, William Ngeleja.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com