1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini

Zainab Aziz
12 Desemba 2018

Wahariri wanazungumzia juu ya kutapatapa kwa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May akitafuta kuungwa mkono nje ya Uingereza ili awatulize wabunge wa nchi yake na hapo jana alifanya ziara nchini Uholanzi na Ujerumani.

https://p.dw.com/p/39vmN
Brüssel Theresa May, Premierministerin Großbritannien
Picha: Reuters/D. Martinez

Frankfurter Allgemeine

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine anasema ni rahisi kutambua kwa nini Theresa May amekutana na viongozi wa nchi hizo mbili. Ujerumani na uholanzi zina mahusiano ya kiuchumi  ya ndani na Uingereza. Ndiyo kusema nchi hizo mbili hazitanufaika ikiwa Uingereza itajiondoa Umoja wa Ulaya bila ya mkataba. Kwenye mazungumzo yake na viongozi wa Ujerumani na Uholanzi, huenda bibi May aliyasikia maneno ya kumpa moyo na kumliwaza. Hata hivyo ukweli ni kwamba  mazungumzo juu ya Brexit yanafanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya. Na hivyo basi litakuwa kosa kwa Theresa May kufikiria kwamba ataweza kuuteteresha msimamo wa nchi za Umoja wa Ulaya kwa kuzishinikiza baadhi ya nchi fulani.

Müchner Merkur

Mhariri wa gazeti la Münchner Merkur anatilia maanani kwamba waziri mkuu wa Uingereza ametambua kuwa nchi za Umoja wa Ulaya haziwezi kugawanyika juu ya suala la Brexit, hata kabla ya  kufanyika mkutano wa mjini Brussels. Mhariri huyo anafafanua kwa kusema, hakuna anayetaka kuona vurumai inayoweza kusababishwa na Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya bila ya mkataba. Na kwa hivyo Theresa May anatumai jinamizi la vurumai za kiuchumi litawafanya wabunge wa nchi yake wauunge mkono mpango wake juu ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya. Njama ya kuahirisha kura ya mpango huo hadi mwezi Januari itawaweka wabunge wa nchi yake chini ya shinikizo. Hata hivyo tarehe 29, Machi mwaka ujao itakuwa siku ambapo Uingereza itapaswa kujiondoa Umoja wa  Ulaya.

Die Welt

Gazeti la Die Welt  linatoa maoni juu ya hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ya Ulaya juu ya mpango wa Benki Kuu ya Ulaya ECB wa kununua hati fungani za serikali kadhaa za nchi za Ulaya. Mahakama hiyo imesema katika hukumu yake kwamba mpango wa beki hiyo ulikuwa sahihi.   Swali iwapo benki kuu inaweza kununua hatifungani kwa kiwango kikubwa limejibiwa na mahakama kuu ya Ulaya kwa niaba ya benki kuu ya Ulaya ECB. Hatua kama hiyo inaweza kuchukuliwa na mahakama kuu na ni ya kawaida katika ulimwengu wa benki kuu, hata hivyo Majaji wa ngazi ya juu huko mjini Karlsruhe awali walikuwa na wasiwasi juu ya ununuzi wa hatifungani hizo kama bado ungelizihusisha fedha za umma kwa njia ya mlango wa nyuma na ndipo ilipoamua kuipeleka kesi hiyo kwenye mahakama kuu ya Ulaya. 

Nordwest 

Mhariri wa gazeti la Nordwest anazungumzia juu ya mwitikio uliotolewa na rais rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa wanaharakati wa vizibao vya manjano. Anasema uamuzi aliopitisha ni sawa lakini mhariri huyo  anatahadharisha kwa kusema ni sahihi kwa rais Macron kupunguza kodi lakini anapaswa kukumbuka kwamba punguzo hilo lazima ligharamiwe, kwa njia ya kupunguza mfuko wa kijamii la sivyo haitawezekana kulipia huduma. Na hicho ndicho anachokifanya. Anaitumbukiza nchi yake katika mgogoro, ambao vinginevyo alitaka kuuepuka na pana hatari ya kuzitumbukiza nchi nyingine za Umoja wa Ulaya kwenye mgogoro huo.

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Iddi Ssessanga