Magazetini Ujerumani | Magazetini | DW | 04.11.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Magazetini Ujerumani

Matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Marekani na mkutano juu ya jitahada za kuwajumuisha wahamiaji katika maisha ya jamii ya Kijerumani ni baadhi ya mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo hii.

Basi tukianza na pigo alilopata Obama na chama chake cha Demokratik, gazeti la LANDESZEITUNG linasema:

"Hata kabla ya uchaguzi kufanyika, ilikuwa wazi kuwa Obama atapata pigo kubwa. Kuna mengi aliyofanya vizuri na ametekeleza baadhi ya ahadi alizotoa wakati wa kugombea urais. Lakini Obama analaumiwa kuhusu idadi kubwa ya wakosa ajira na uchumi unaodorora nchini humo, licha ya kuwa huo ni mzozo aliourithi kutoka kwa mtangulizi wake George W. Bush. Hata hivyo Obama hana budi kushughulikia zaidi matatizo hayo ikiwa anataka kuchaguliwa kwa awamu ya pili. Kwani hakuna kinachowatia zaidi wasiwasi Wamarekani kuliko uchumi ulio dhaifu."

Lakini gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG linasema:

"Obama wala hana haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu uchaguzi utakaofanywa miaka miwili kutoka sasa. Kwani baadhi ya marais waliomtangulia walishindwa vibaya sana katika uchaguzi kama huu, lakini walikujashinda miaka miwili baadae. Kwani hata katika suala hilo Wamarekani ni wahafidhina sana."

Tukiendelea na mada hiyo hiyo gazeti la MANNHEIMER MORGEN linaeleza hivi:

"Wamarekani wamempa funzo Barack Obama. Sasa hana budi kutafuta jibu la maana kwa somo hilo kali. Lakini hata Warepublikan waliokuwa wakingángania msimamo wa kupinga kila siasa ya serikali ya Obama, wanapaswa kubadili msimamo huo. Kwani matokeo ya uchaguzi huo yamebainisha matakwa ya wapiga kura yaani, vyama vyote viwili vikuu viwajibike na kufanya kazi pamoja. Marekani haiwezi kukwamisha siasa za ndani wakati ikibaliwa na matatizo."

Sasa tunatupia jicho mada yetu ya pili inayohusika na mkutano kuhusu jitahada za kuwajumusha wahamiaji katika maisha ya jamii ya Kijerumani. Kwa maoni ya gazeti la OLDENBURGISCHE VOLKSZEITUNG hakuna shaka yo yote ile kuwa mkakati wa kitaifa ndio ufumbuzi sahihi wa kuwajumusha wahamiaji kwa haraka na bora zaidi. Linaongezea:

"Mbali na kuwawajibisha wahamiaji kujijumuisha katika jamii, mradi huo unabainisha haja ya jamii pia kuwa tayari kuwa na maingiliano na watu wenye asili ya kigeni. Makosa ya zamani hayawezi kukanwa. Mengi yaliahidiwa. Kutakuwa na utaratibu utakaosawazisha makosa yatakayojitokeza - matokeo ya jitahada mpya yanaweza kutegemewa katika muda usio mrefu kutoka sasa."

Mwandishi:Martin,Prema/DPA

Mpitiaji: Charo,Josephat