Magazetini Ujerumani | Magazetini | DW | 10.08.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Magazetini Ujerumani

Kuongezeka kwa bidhaa zinazoagizwa na Ujerumani kutoka nje na kufungwa kwa msikiti mmoja mjini Hamburg ni baadhi ya mada zilizoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya leo hii ya Jumanne nchini Ujerumani.

Tutaanza na gazeti la SCHWÄBISCHE ZEITUNG linalouliza iwapo bidhaa rahisi za Kichina zitafurika nchini Ujerumani?

"Jawabu ni la, kwani uchumi imara wa Ujerumani ndio unaoifanya China kuwa muuzaji mkubwa wa bidhaa zake nchini Ujerumani. Kwa sehemu kubwa nchi zinazoinukia kiuchumi, kama vile India, Brazil na hata China zinafanikiwa kuuza bidhaa nyingi katika nchi za nje kwa kutumia mashine za Kijerumani kutengenezea bidhaa zao. Na hali hiyo haitobadilika ikiwa Ujerumani itaendelea kufuata msingi ulioleta mafanikio kwa karne kadhaa: yaani kuwa nchi yenye sera za masoko huria katikati ya bara la Ulaya na iliyo na ubunifu unaoweza kutumiwa kutengeneza bidhaa bora - hata kwa wateja wa Kichina."

Gazeti la GENERAL ANZEIGER likiandika juu ya mada iliyosababisha midahalo mikali nchini Ujerumani kuhusu wahalifu 80 wa ubakaji wanaomaliza vifungo vyao linasema:

"Polisi kuendelea kuwafuatilia wahalifu mchana na usiku, baada ya kuachiliwa kutoka jela, sio suluhisho.Hata kuwafunga chombo cha elektroniki mguuni itakuwa changamoto kubwa kwa polisi. Vile vile, haiwezekani kuirejesha Ujerumani katika enzi ya kale kwa kuwafedhehesha watu hao hadharani. Kuchapisha picha, majina na anuani za watu hao katika mtandao wa intaneti ni ukiukaji wa katiba ya nchi. Kwani hapo ipo hatari ya wenyeji kuchukua sheria mikononi mwao na kumuadhibu jirani huyo alieachiwa kutoka jela.Kilichobaki ni kutafuta suluhisho litakalohakikisha usalama na wakati huo huo kufuata sheria ya nchi."

Hiyo ni mada tete na jawabu la serikali ya Ujerumani linatuliza moyo, lasema gazeti la WESTFÄLISCHE ANZEIGER kuhusu pendekezo la kuwataja wahalifu wa ubakaji katika mtandao,lililopingwa.

"Hata hivyo,wale wanaoshikilia kuwataja wahalifu hao wa ubakaji hawakuridhika na jawabu la serikali. Bila shaka wanasiasa wanapaswa kuzingatia wasiwasi wa umma usiotaka kuwa na jirani mbakaji. Hapo,kuna njia moja tu,yaani kunahitajiwa nyenzo mpya - sio jela wala kuwafuatlia wahalifu hao usiku na mchana. Kwa njia hiyo, pande zote mbili zitaridhika."

Tukibadili mada gazeti la KIELER NACHRICHTEN linasema:

"Hatua iliyochukuliwa kuufunga msikiti ni ishara wazi kuwa hakuna eneo linaloweza kutumiwa kinyume na sheria. Kuambatana na sheria za vyama, vyama vinaweza kupigwa marufuku vinapokwenda kinyume na msingi wa demokrasia na hata kinyume na maadili ya jamii. Na msikiti uliofungwa umekiuka yote hayo kwani kituo kilichodaiwa kuwa ni cha utamaduni kilikuwa kitovu cha kuwaanda Waislamu wenye itikadi wanaokuwa tayari kujitolea muhanga. Na hayo yote yalitendeka kwa kutumia dini."

Na hapo tunakamilisha yale yaliyogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo hii.

Mwandishi .P.Martin/DPA

Mhariri: Charo, Josephat

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com