Magazetini Ujerumani | Magazetini | DW | 05.05.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Magazetini Ujerumani

Miongoni mwa habari zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu ni pendekezo la chama cha CSU ambacho ni chama ndugu cha CDU,kuwapunguzia watu wa tabaka ya kati kodi ya pato.

Bila shaka mazungumzo kati ya wawakilishi wa Dalai Lama pamoja wajumbe wa serikali ya China yamepewa umuhimu katika magazeti ya leo.Basi tutaanza na Südwest Presse.

Naam gazeti hilo linasema lengo la chama cha CSU ni dhahiri,kwa hivyo linakera.Kwani uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa chama hicho kimepoteza umaarufu wake na sasa ndio kimegusia mada yakuvutia,yaani kuwapunguzia raia mzigo wa mfumko wa ughali wa maisha.Kwa maoni ya CSU,mfuko wa serikali umejaa kwa faida iliyopatikana kutokana na kodi ya ongezeko la thamani ya bidhaa na hata bei ya petroli.Kwa hivyo wananchi wapunguziwe mzigo wa ughali wa maisha.

Lakini gazeti la Westdeutsche Allgemeine Zeitung linasema,ni rahisi sana kutia mashakani pendekezo la mwenyekiti wa CSU Erwin Huber.

Likiendelea linauliza,kwanini chama cha CSU kimefikria kutoa pendekezo hilo hivi sasa?Wakati ambapo chama hicho kimepata matokeo mabaya kabisa katika uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni?Na kwanini pendekezo hilo linachomoza muda mfupi kabla ya uchaguzi katika jimbo la Bavaria,chama cha CSU kikikabiliwa na kitisho cha kupoteza kura?Inasikitisha kuwa mwenyekiti wa CSU Erwin Huber amewapa wapinzani wake chambo cha kumshambulia kwa urahisi.

Rheinische Post linasema,mwanya kati ya masikini na matajiri unazidi kuwa mkubwa.Likifafanua zaidi linaeleza hivi:

Katika mwaka 2000 nchini Ujerumani idadi ya watu wa tabaka ya kati ilikuwa milioni 49,na miaka sita baadae idadi hiyo imepunguka hadi milioni 44.Idadi ya masikini inaongezeka,lakini matajiri pia wameongezeka.

Usemi kuwa wakati wa shida mtu anapaswa kukaza mkanda ili apate kunufaika wakati wa neema,hauna maana tena kwa Wajerumani hivi sasa.

Kwa hivyo serikali inapaswa kuchukua hatua ili umma uweze kuwa na matumaini ama sivyo,tena nchini humu kutarejea jamii yenye tabaka mbali mbali linaonya gazeti la Rheinische Post.

Sasa tunapindukia mengine muhimu yaliyotokea nje ya Ujerumani.Michezo ya Olimpiki ikikaribia,ndio macho ya ulimwengu yanazidi kuelekezwa China ambayo hivi karibuni ililaumiwa kwa jinsi ilivyomaliza ghasia zilizozuka Tibet katika mwezi Machi.Tukibakia na Rheinische Post,gazeti hilo linasema:

Mazungumzo kati ya China na wawakilishi wa kiongozi wa kidini wa Tibet,Dalai Lama ni matokeo ya shinikizo kubwa la jumuiya ya kimataifa.Hata hivyo,mtu asijidanganye kuwa kutakuwepo matokeo ya kuridhisha.Kwani China inajikuta chini ya shinikizo kubwa na kwa vyo vyote vile haitaki kuona suala la Tibet likigubika Michezo ya Olimpik itakayofanywa Beijing mwezi Agosti.

Rhienische Post likiendelea linasema,mazungumzo kati ya China na wajumbe wa Dalai Lama yatakuwa na maana ikiwa pande zote mbili zitakuwa tayari kuafikiana.Tangu hapo mwanzoni Dalai Lama ameeleza wazi wazi kuwa anachotaka ni uhuru wa kitamaduni kwa Watibet yaani anataka kuona utamaduni wa Watibet ukihifadhiwa na si jingine lolote zaidi.Yeye amepinga kabisa shutumu za Beijing kuwa anataka uhuru wa Tibet.Kwa hivyo itakuwa vigumu kutazamia suluhu na hali China humuita Dalai Lama adui wa taifa.Kwa maoni ya Rheinische Post,suala la Tibet kwa vyo vyote vile litagubika Michezo ya Olimpiki-na hilo ndio tatizo kubwa la China.