Magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii. | Magazetini | DW | 29.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii.

Magazeti ya Ujerumani yasema kiongozi wa upinzani Macky Sall ni matumani ya vijana nchini Senegal.Magazeti hayo pia yameandika juu ya matukio ya nchini Mali baada ya askari kutwaa mamlaka

Macky Sall ,matumaini ya vijana nchini Senegal

Macky Sall matumaini ya vijana nchini Senegal

Gazeti la"die tageszeitung" limeandika juu ya matukio ya nchini Mali.

Chini ya kichwa cha habari kinachosema mwisho wa kigezo cha demokrasia nchini humo gazeti hilo limeripoti kwamba wanajeshi walioasi wametwaa mamlaka nchini Mali kwa sababu wamesema wamechoshwa na jinsi serikali ya Rais Amadou Toumani Toure ilivyokuwa inaukabili mgogoro wa kaskazini mwa nchi.

Ripota wa gazeti la"die tageszeitung"amearifu kuwa mapigano makali yalitokea katika mji mkuu wa Mali, Bamako hapo jumatano.Na siku iliyofuatia askari walioasi walitangaza kwa njia ya radio ya serikali kuwa wametwaa mamlaka ya uongozi na kwamba wameunda kamati ya kitaifa ya kuleta demokrasia nchini.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" liemandika juu ya raundi ya pili ya uchaguzi nchini Senegal. Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba Kiongozi wa upinzani Macky Sall ni ishara ya matumaini kwa vijana wa Senegal. Gazeti la "Suddeutsche Zeitung" linatilia maanani katika makala yake kwamba vyama vya upinzani viliwaandaa wapiga kura na kuwasilisha ujumbe mmoja tu, kwamba Abdoulaye Wade lazima aondoke.!

Gazeti la "die tageszeitung" limeandika juu ya ukanda wa Video wenye filamu inayomwoshenya kiongozi wa kundi la wauaji la Lord's Resistance Army la Uganda ,Joseph Kony. Filamu hiyo imetifua tufani nchini Uganda. Katika taarifa yake juu ya athari za filamu hiyo nchini Uganda ripota wa gazeti la"die tageszeitung"anaarifu kwamba maoni ya watu nchini Uganda juu ya filamu hiyo yamegawanyika. Katika mji mdogo wa Lira ambako kwa miaka mingi waasi wa Lord's Resistance Army walikuwa wanawateka nyara watoto na kuviteketeza vijiji,mamia ya watu waliokuwa wanaitazama filamu hiyo walianza kutupisha mawe.

Gazeti la"die tageszeitung"limearifu kuwa filamu juu ya Kony pia imeshutumiwa na viongozi wa serikali ya Uganda. Waziri Mkuu wa nchi hiyo Amama Mbabazi amesema Uganda haihitaji mtandao wa internet ili kuwa macho juu ya Kony. Gazeti hilo limemkariri Waziri Mkuu huyo akisema kuwa Kony hayupo Uganda!

Shirika moja la hisani nchini Marekani linaloitwa "Invisible Children" liliiweka filamu hiyo juu ya Kony kwenye mtandao wa kijamii wa You Tube ili kutoa mwito kwa majeshi ya Uganda kwa kushirikiana na Marekani wa kumkamata Kony.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alifanya ziara nchini Angola mwezi juni mwaka jana. Katika ziara hiyo Kansela Merkel alishiriki katika kuuzindua mradi wa ujenzi wa ukumbi wa uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Angola , Luanda.Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Der Tagesspiegel". Lakini gazeti hilo linasema mradi huo sasa unakabiliwa na matatizo.

"Der Tagesspiegel" limeripoti kwamba Kansela Merkel aliweka jiwe la msingi kuuzindua ujenzi wa mradi wa pamoja baina ya kampuni ya Angola na ya Ujerumani inayoitwa LSG. Lengo lilikuwa kuziimarisha huduma zilizokuwa zinatolewa na kampuni ya Angola, inayoitwa Maboque. Kampuni hiyo imekuwa inatoa huduma kwa muda wa miaka 15 ikiwa na wafanyakazi 940. Lakini tokea kuanzishwa mradi wa pamoja na kampuni ya Ujerumani,nafasi za wafanyakazi 400 sasa zimo mashakani. Gazeti la"Der Tagesspiegel" linasema badala ya kumletea umaarufu, mradi huo sasa utamfanya Kansela Merkel ajute.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman