1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magari ya kijeshi ya Urusi yaonekana karibu na Ukraine

Sudi Mnette
23 Februari 2022

Kampuni moja ya kibinafsi ya Kimarekani-Maxar Technologies imesema picha zilizonaswa kwa setilaiti zinaonesha zaidi ya magari 100 ya kijeshi na idadi kubwa ya mahema kusini mwa Belarus karibu na mpaka wa Ukraine

https://p.dw.com/p/47Rkm
Ukraine Rauchsäule über einem beschossenen Kraftwerk nähe Luhansk
Picha: ARIS MESSINIS/AFP via Getty Images

Taswira hizo pia zinaonesha maeneo mapya ya hospitali pamoja na idadi kubwa ya vifaa vilivyokuwa vikipelekwa katika eneo la kusini mwa Urusi, karibu na mpaka wake na Ukraine. Hata hivyo kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, limeshindwa kuhakiki picha hizo.

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameamuru majeshi ya taifa lake kuingia katika eneo la mashariki mwa Ukraine kwa kile alichoeleza kulinda amani baada ya serikali yake kutambua uhuru wa wanaotaka kujitenga katika majimbo ya Donetsk na Luhansk.

Kwa mujibu wa Maxar malori makubwa ya kusafrisha zana nzito yametumika kusafirisha vifaru, mizinga na vitu vingine vizito, ambavyo vimeshuhudiwa karibu na mpaka wa Ukraine magharibi mwa Urusi, hatua ambayo inatajwa kwenda sambambaa na kuwasili kwa wanajeshi katika maeneo hayo.

Serikali ya Ukraine imesema vikwazo dhidi ya Urusi ni mwimba mchungu.

Russland | Russische Militärübungen
Mazoezi ya kijeshi kati ya Belarus na UrusiPicha: AP/picture alliance

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba amechungu vikwazo vikali dhidi ya Urusi kutokana na mzozo baina ya taifa lake na Urusi. Katika mkutano wake wa waandishi wa habari wa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Antony Blinken amesema vikwazo hivyo vimelenga eneo mahususu na vyenye machungu sana.

Marekani Jumatatu imeiwekea vikwazo vyenye kuhusiana na uchumi Urusi kutokana na hatua yake katika majimbo ya Donetsk na Luhansk huko mashariki mwa Ukraine. Katika mkutano wao huo wa pamoja mawaziri hao wamesema hakuna jambo dogo, la wastani au uvamizi mkubwa. Uvamizi ni uvamizi.

Mkuatano uliotarajiwa kati ya marais Biden wa Marekani na Putin  wa Urusi umesitishwa.

Wakati huohuo Waziri Blinken amesema mpango wa Rais Putin wakati wote ulikuwa kuivamia Ukraine, kuidhibiti Ukraine na watu wake, kuivuruga demokrasia ya Ukraine, kuvuruga uhuru wa uongozi wa taifa hilo kwa shabaha ya kurejesha Ukraine kuwa sehemu ya Urusi.

Aidha Ikulu ya Marekani imefuta mpango wa mkutano wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Joe Biden wa Marekani. Msemaji wa Biden Jen Psaki amesena kwa ujumla kiongozi huyo wa Marekani kwa sasa anafungua majadiliano ya kidiplomasia na mazungumzo katika kiwango cha juu lakini sio sasa katika kipindi ambacho Urusi inazidisha hali ya mzozo wa Ukraine, akiongeza kusema sio wakati muafaka.

Mkutano wa ana kwa ana kati ya Biden na Putin umekuwa katika mjadala mkubwa katika siku za hivi karibuni. Kimsingi Biden alikubali kukutana na Putin na serikali ya Urusi ilikwisha onesha utayari wa jambo hilo. Lakini msemaji wa ikulu ya Marekani ameongeza kwa kusema hakukuwa na ratiba maalumu ya mkutano mwingine wa marais hao wawili.

Kuhusu suala hilo kwa ufafanuzi zaidi limepangwa kujadiliwa Alhamis kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na mweziwe wa Urusi Sergei Lavrov. Lakini mkutano huo kwa sasa umesitishwa.