1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magaidi wahukumiwa vifungo virefu jela.

Abdu Said Mtullya4 Machi 2010

Kundi la magaidi linaloitwa "Sauerland" lahukumiwa Düsseldorf.

https://p.dw.com/p/MJs6
Magaidi wa Ujerumani waliohukumiwa vifungo virefu jela.Picha: picture-alliance/dpa

Watu wanne waliokiri kula njama za kupanga mashambulio ya kigaidi katika sehemu zinazowahusu Wamarekani nchini Ujerumani wamehukumiwa adhabu ya vifungo virefu jela.

Watu hao wanne, waislamu wenye itikadi kali, walihukumiwa vifungo vya hadi miaka 12 jela na mahakama ya mjini Düsseldorf mapema leo.

Waislamu hao wenye siasa kali walipatikana na hatia ya kupanga njama za kufanya mauaji na hatia ya kuwamo katika kundi la kigaidi.

Waliohukumiwa ni Fritz Gelowicz na Daniel Schneider, waliopewa adhabu ya miaka 12 jela kila mmoja. Wote wawili ni Wajerumani waliosilimu.

Wengine ni Adem Yilmaz mwananchi wa Uturuki aliepewa adhabu ya kifungo cha miaka 11 jela, na mwengine ni Atilla Seleck, Mjerumani mwenye asili ya kituruki. Yeye amehukumiwa miaka mitano kwenda gerezani.

Watu hao wamo katika kundi linaloitwa Sauerland.

Na wote walikiri kwamba walikuwa na mpango wa kufanya mashambulio ya mabomu katika sehemu zinazohusiana na Wamarekani nchini Ujerumani.

Mnamo mwaka 2007 walikuwa wamepiga hatua katika matayarisho ya kufanya mashambulio ya mabomu ya kilogramu 250 kwa kutumia magari matatu.

Msemaji wa mahakama ya mjini Düsseldorf, Ulrich Egger, alieleza baada ya hukumu kutolewa kwa watu hao kwamba kesi hiyo imetoa mwanga juu ya muundo wa magaidi wa kiislamu wenye itikadi kali nchini Ujerumani,na hasa imetoa mwanga juu ya Wajerumani wanaojiunga na uislamu wa siasa kali na kutenda uhalifu.

Watu hao walikamatwa mnamo mwaka 2007 katika kijiji kimoja cha Sauerland, Oberschledorn baada ya kuchunguzwa kwa wiki nzima.

Walikuwa na mpango wa kuunda mabomu kwa lengo la kushambulia viwanja vya ndege, sehemu za burudani na kambi za kijeshi za Marekani nchini Ujerumani.

Msemaji wa mahakama ya mji wa Düsseldorf ameeleza kuwa magaidi walikuwa wanapanga kuwaua watu wasiopungua 150 nchini Ujerumani na hasa Wamarekani.

Mwandishi/Mtullya Abdu dpa/ZA

Mhariri: Miraji Othman