1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafia yauwa Duisburg

Oummilkheir15 Agosti 2007

Wataliana sita wapigwa risasi kichwani katika mji tulivu wa Duisburg- Magharibi ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/CHjj
Maiti ya mhanga mmoja wa mashambulio ya Duisburg
Maiti ya mhanga mmoja wa mashambulio ya DuisburgPicha: AP

Watu sita,wote wanaume, wamegunduliwa wameuliwa kwa kupigwa risasi kichwani katika kituo cha usafiri wa reli mjini Duisburg katika jimbo la North Rhine Westphalia-NRW,usiku wa jana kuamkia leo.

Wakiarifiwa na mpita njia aliyesikia risasi zikifyetuliwa,polisi wa Duisburg walioharakisha kufika mahala tukio hilo lilikojiri,saa nane na nusu za usiku ,jana kuamkia leo,wamegundua miili ya watu hao sita ndani na nje ya magari mawili , karibu na mkahawa wa kitaliana “Bei Bruno”si mbali na kituo cha usafiri wa reli.Watano walikua wameshakufa na wasita amefariki alipokua njiani kupelekwa hospitali.

Duru za polisi zimesema leo asubuhi,wahanga wote sita ni wataliana wenye umri wa kati ya miaka 16 na 39. Kwa mujibu wa msemaji wa polisi wahanga wote sita wamepigwa risasi kichwani.

Wahanga wanasemekana walikua ndani ya magari mawili VW GOLF na jengine chapa ya Opel-yote mawili yamesajiliwa mjini Duisburg.Polisi wanategemea filamu iliyonaswa na kamera zilizowekwa kwenye maduka ya eneo hilo ili kujua zaidi kilichotokea.

Jamaa za wahanga wanahojiwa na polisi na mbwa wa upelelezi wameshapelekwa katika eneo hilo.Magari yote mawili walimokuwepo wahanga hao,ambayo yamefyetuliwa risasi na kugeuzwa kumto yanafanyiwa uchunguzi wa kina.

Inaaminiwa kabla ya mashambulio,wahanga hao walikuwa katika mkawaha wa Bei Bruno.Watu wawili,wasiojulikana walionekana karibu na hapo,lakini haijulikani kama wanahusika au la na mauwaji hayo.

Wakaazi wa Duisburg,mji tulivu kabisa katika eneo la mto Ruhr wameshtushwa na kisa hicho ambacho hakijawahi kutokea katika mji wao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Italy Ansa wataliana hao sita waliouliwa-Duisburg, magharibi ya Ujerumani pengine ni wafuasi wa kundi la wahalifu wa Mafia “Ndrangheta-“-la Calabria.

Kwa mujibu wa shirika hilo la habari,kituo cha polisi cha Reggio Calabria kwa ushirikiano pamoja na idara za polisi ya kimataifa Interpol mjini Roma na Polisi wa Duisburg wamegundua kwamba wahanga hao sita wanatokana na makundi mawili ya “Ndrangheta” yanayohusika na visa kadhaa vya kulipiziana kisasi.

“Ni tukio lisilokua na mfano,ni mara ya kwanza kutendeka katika nchi ya kigeni” amesema naibu mkurugenzi wa Polisi ya Italy Luigi De Sena-ambae ni meya wa zamani wa Reggio Calabiria.

Duru za polisi ya Italy zinasema wahanga wa mashambulio ya Duisburg wanatokea katika kundi la Pelle-Romeo linalogombana na kundi jengine la mafia Strangio-Nirta na kwamba waliowauwa wametokea Calabaria.

Ofisi kuu ya polisi ya Italy inapanga kutuma wataalam hii leo mjini Dusiburg kusaidiana na polisi wa Ujerumani katika utafiti wao.