1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wafuasi wa Navalny wakamatwa Urusi

31 Januari 2021

Zaidi ya watu 2,100 wamekamatwa leo Jumapili wakati wa maandamano yaliyofanyika kwenye miji mbalimbali nchini Urusi kushinikizwa kuachiwa kwa kiongozi wa upinzani aliye kizuizini Alexei Navalny.

https://p.dw.com/p/3odR5
Russland | Protest gegen die Festnahme von Alexei Nawalny
Polisi wakimbeba msobemsobe mmoja ya waandamanaji.Picha: Alexander Zemlianichenko/AP Photo/picture alliance

Maandamano zaidi yanatarajiwa kwenye mji mkuu Moscow, na tayari mamlaka za mji huo zimeamuru kufungwa kwa vituo vya treni na kuweka vizuizi kwenye mitaa inayozunguka Ikulu ya Kremlin.

Maelfu ya watu wamejitokeza kushiriki maandamano hayo ya kumuunga mkono Navalny na kulaani uamuzi wa mamlaka za Urusi kumuweka korokoroni.

Kulingana na kundi linalofuatilia hali ya mambo nchini Urusi, hadi mchana wa leo polisi ilikuwa imewakamata waandamanaji 2,100. Shirika la Habari la Reuters limeripoti mjini Moscow pekee watu 100 wamekamatwa.

Polisi ililazimika kuufunga uwanja wa Lubyanka ulio karibu na Ikulu ya Kremlin eneo ambalo waandamanaji walipanga kukusanyika. Kutokana na hatua hiyo, waandaaji wa maandamano hayo waliwahimiza wafuasi wao kujikusanya kwenye uwanja mwingine wa wazi mjini Moscow.

Polisi wamejaribu kuzuia maandamano yasifanyike 

Mwandishi wa Habari wa DW mjini Moscow Emily Sherwin amesema mamlaka za mji huo zimekwenda mbali zaidi na hata kuzuia maandamano yasifanyike: " Wameweka vizuizi kwenye eneo kubwa la mji mkuu...wamefunga barabara, wamebadili njia za mabasi ya abiria, vituo saba vya treni vimefungwa" amearifu Sherwin.

Russland | Protest gegen die Festnahme von Alexei Nawalny
Licha ya baridi kali, waandamanaji walijitokeza kwenye miji mbalimbali ya Urusi Picha: Valentin Egorshin/AP Photo/picture alliance

Sherwin pia ameripoti kuwa kutokana na vizuizi hivyo waandamanaji wameshindwa kuingia katikati ya mji na "wasaidizi wa Navalny wametangaza maeneo mapya ya watu kukutana na inaonekana mamlaka [za mji wa Moscow] na waandamanaji watakuwa wakicheza mchezo wa paka na panya"

Maandamano ya kwanza yamefanywa kwenye mji wa mashariki mwa nchi hiyo wa Vladivostokambako polisi wamewazuia waandamanaji kuingia katikati ya mji. Mkanda wa video umeonesha watu wakiunganisha mikono na kupaza sauti "Putin ni mwizi" wakati wakikusanyika licha ya kuwepo baridi kali inayopindukia nyuzi -13. Watu 100 wamekamatwa kwenye mji huo.

Kwengineko maelfu ya watu wamehudhuria mkusanyiko kwenye mji wa kaskazini mwa jimbo la Siberia wa Novosibinsk, ambako watu 90 wametiwa kizuizini. Vyombo vya habari vya eneo hilo pia vimeripoti kutokea makabiliano kati ya polisi na waandamanaji katikati ya mji wa Chelyabinsk kulikokuwa pia kunafanyika maandamano.

Mamlaka za Urusi zasema maandamano hayo siyo halali

Maelfu ya watu tayari walikamatwa wiki moja iliyopita waliposhiriki maandamano ya nchi nzima kumuunga mkono Navalny aliyekamatwa na kuwekwa kizuizini mnamo Januari 17 muda mfupi baada ya kuwasili mjini Moscow akitokea Ujerumani.

RUSSIA-POLITICS-OPPOSITION-DETAIN
Alexei NavalnyPicha: Dimitar Dilkoff/APF/Getty Images

Mkosoaji huyo mkubwa wa utawala wa rais Vladimir Putin wa Urusi alipewa sumu ya kuharibu mfumo wa fahamu jimboni Siberia Agosti mwaka jana na alilazimika kupelekwa mjini Berlin kupatiwa matibabu.

Polisi nchini Urusi walitahadharisha kuwa maandamano ya leo Jumapili ni kinyume cha sheria na yatavunjwa.

Ubalozi wa Marekani nchini Urusi umewaonya raia wake nchini humo juu ya uwezekano wa kukamatwa, ukiorodhesha maeneo na muda maandamano yamepangwa kufanyika, hatua ambayo imeikasirisha wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi.