1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waukimbia mji wa Sirte

3 Oktoba 2011

Maelfu ya watu wanaukimbia mji wa Sirte, alikozaliwa kiongozi wa Libya aliepinduliwa madarakani, Mummar Gaddafi leo hii, wakati waasi wakijiandaa kufanya shambulio kubwa kwa mji huo.

https://p.dw.com/p/Ron5
Wananchi walioukimbia mji wa Sirte nchini Libya Jumapili ya tarehe 2 Oktoba 2011.
Wananchi walioukimbia mji wa Sirte nchini Libya Jumapili ya tarehe 2 Oktoba 2011.Picha: AP

Inaelezwa kwamba hali katika mji huo ni mbaya sana na kwamba raia wamekuwa wakijeruhiwa na wengine kupoteza maisha yao kutokana na uhaba wa vifaa vya matibabu.
Raia wamekuwa wakitumia fursa ya usitishaji wa mapigano wa siku mbili uliotangazwa na Baraza la Taifa la Mpito nchini Libya kuwaruhusu kuyakimbia mapigano hayo, ingawa raia wanaotoka katika mji huo wanasema hawafahamu kitu kuhusu usitishaji huo wa mapigano na kwamba mashambulio ya risasi yamekuwa yakiendelea. Usitishaji huo wa mapigano ulipangwa kumalizika jana ambapo waasi wamesema walikuwa wanajiandaa kwa shambulio kubwa dhidi ya wapiganaji wa Gaddafi ambao wamekuwa wakiweka upinzani mkali katika mji huo wa bandari kwa wiki kadhaa sasa.

Wakaazi wa mji huo wenye idadi ya watu wanaokadiriwa kufikia 70,000 wanakimbia kwenye magari yaliojazana watu, wengi wao wakiwa wamekalia mizigo yao kwenye magari makubwa ya mizigo.

Raia wakisheherekea vikosi vya serikali mpya ya Libya karibu na mji wa Sirte
Raia wakisheherekea vikosi vya serikali mpya ya Libya karibu na mji wa SirtePicha: dapd

Watu waliokuwa wamejeruhiwa katika mapigano kwenye mji huo wa Sirte uliozingirwa na wapiganaji wa serikali mpya ,wamekuwa wakipoteza maisha yao wakiwa kwenye meza za operesheni kutokana na hospitali kuishiwa na mafuta.

Mtu mmoja ameliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters, kwamba ameshuhudia mtoto wa miaka 14 akifariki kwenye meza ya operesheni kwa sababu umeme ulikatika wakati akifanyiwa operesheni.

Mashirika ya misaada yameilezea hali ilioko kwenye mji huo kuwa mbaya sana.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema raia wanajikuta katikati ya mapigano na kwamba chakula, maji na umeme vinamalizika.

Wafanyakazi wa misaada kutoka Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu ambao walifikisha misaada yao ya matibabu kwa mji wa Sirte hapo Jumamosi walikuwa wameshindwa kuifikia hospitali hiyo kutokana na mapigano ya risasi.

Wasi wasi mkubwa zaidi uko katika hospitali hiyo kuhusiana na maafa ya kibinadamu katika mji huo.

Inaelezwa kuwa wagonjwa wanakufa kila siku kwa kukosa gesi ya oxygen.

Waasi wamekuwa wakijaribu kwa zaidi ya wiki mbili kuuteka mji wa Sirte mojawapo ya ngome kuu mbili za mwisho za Gaddafi nyengine mji wa kaskazini magharibi wa Bani Walid.

Mwandishi: Mohamed Dahman/RTRE/dpa

Mhariri:Miraji Othman