1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madrid yaizamisha PSG, Liverpool yaicharaza Porto

Bruce Amani
15 Februari 2018

Cristiano Ronaldo alifunga mabao mawili wakati Real Madrid ilipoikandika PSG 3-1. Mjini Porto, Liverpool ilionyesha mchezo mzuri wa kushambulia na kuwabamiza mabingwa wa 2004 5-0 ugenini katika uwanja wao wa nyumbani

https://p.dw.com/p/2ski0
Championsleague Real Madrid vs Paris St Germain
Picha: Reuters/P. Hanna

Real Madrid 3-1 Paris Saint-Germain
(Ronaldo pen 45', 83', Marcelo 86' — Rabiot 33')

Real Madrid ilifunga mabao mawili katika dakika saba za mwisho na kupata ushindi dhidi ya Paris Saint-Germain  katika mji mkuu wa Uhispania.

Zinedine Zidane aliingia katika mchezo huo akiwa chini ya shinikizo kubwa, baada ya timu yake kuwa na matokeo mabya tangu mwanzoni mwa mwka ambayo yamesababisha mabingwa hao mara 12 wa Ulaya kuteremka hadi nafasi ya nne ya msimamo wa La Liga.

Lakini walikuwa ni wageni kutoka Ufaransa waliokuwa na nafasi nzuri katika kipindi cha kwanza na wakati bao la ufunguzi lilifungwa na mabingwa hao watarajiwa wa Ligue 1 sio kitu kilichokuwa kimetarajiwa sana.

Kylian Mbappe alipiga krosi ambayo iliguswa na mguu wa Nacho na kumfikia Adrien Rabiot ambaye alisukuma wavuni kwa ustadi wa hali ya juu na kumzidi maarifa kipa Keylor Navas.

Toni Kroos aliangushwana Giovani Lo Celso katika eneo la adhabu na Cristiano Ronaldo akafunga penalti.

UEFA Championsleague - FC Porto vs Liverpool - Tor Liverpool
Washambuliaji wa Liverpool waliitatiza PortoPicha: Reuters/M. Childs

PSG walijaribu kuudhibiti mchezo lakini Real Madrid waliongeza kasi katika dakika za mwisho mwisho na wakapata bao la tatu kupitia Cristiano Ronaldo, na kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 100 katika Champions League akiwa na klabu moja.

Lakini Madrid hawakuwa wamemaliza kazi. Marcelo aliiunganisha krosi ya Marco Asensio na kombora lake likamgonga nahodha wa PSG Mbrazil Marquinhos na kutumbukia ndani ya wavu, na kuipa Real faida ya wazi kabla ya mchuano wa marudiano  mjini Paris na pia kumuondolea Zidane shinikizo kidogo

Porto 0-5 Liverpool
(Mane 25' 53' 85', Salah 29', Firmino 70')

Liverpool imeuweka mguu mmoja kwenye robo fainali baada ya kuonyesha mchezo wa hali ya juu mjini Porto. Sadio Mane alifungua ukurasa wa magoli wakati alisukuma kombora lililomkwepa kipa Jose Sa.

Dakika nne baadaye vijana hao wa kocha Jurgen Klopp wakaongeza la pili wakati kombora la James Milner liliugonga mlingoti na mpira kuanguka miguuni pa Mohamed Salah, ambaye alifanya mambo yake na kusukuma wavuni bao lake la 30 msimu huu.

Mane aliongeza la tatu baada ya counter attack kali sana kabla ya Roberto Firmino kujiunga na karamu ya mabao alipofunga bao la nne la Liverpool. Mane kisha akafunga kazi na bao la tano la Liverpool.

Mane sasa amejiunga na Michael Owen, Yossi Benayoun na philippe Coutinho kuwa wachezaji pekee kufunga hat trick katika Champions League.

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Josephat Charo