1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madrid na Dortmund kukwaruzana tena

21 Machi 2014

Real Madrid wamepewa fursa ya kulipiza kisasi kichapo walichopewa na Borussia Dortmund msimu uliopita katika nusu fainali ya UEFA Champions League. Timu hizo mbili zimepangwa tena katika robo fainali

https://p.dw.com/p/1BU3r
UEFA Champions League Ziehung 21.03.2014
Picha: Harold Cunningham/Getty Images for UEFA

Mabingwa watetezi Bayern Munich wamepangwa na Manchester United, dimba ambalo litaibua kumbukumbu za fainali yao ya mwaka wa 1999 wakati United ilifunga magoli mawili katika dakika za mwisho mwisho na kupata ushindi wa mabao mawili kwa moja. Paris St Germain watakabana koo na Chelsea wakati Barcelona na Atletico Madrid zote kutoka uhispania zikishuka dimbani katika mpambano unaotarajiwa kuwa mkali.

Mshambuliaji wa BVB Mpoland Robert Lewandowski, aliyefunga magoli yote manne katika ushindi wa Dortmund wa mabao manne kwa moja dhidi ya Real Madrid msimu uliopita, atakuwa nje katika mechi ya kwanza dhidi ya mabingwa hao mara tisa wa ulaya ili kutumikia adhabu ya kadi nyingi za njano..

Afisa Mkuu mtendaji wa BVB Hans-Joachim Watzke alisema baada ya Lewandowski kupewa kadi ya njano katika mechi y amkondo wa pili dhidi ya Zenit St Petersburg kuwa “hilo ni pigo kubwa. Yeye ni mchezaji mzuri. Ulikuwa uamuzi wa kushangaza”.

Amesema Real ni kikosi kikali lakini watajitahidi kila wawezavyo kwa sababu katika awamu hii hakuna timu yoyote dhaifu. Bayern nao ambao wanalenga kutwaa mataji ya Champions League, Bundesliga na Kombe la Shirikisho, kwa msimu wa pili mfululizo, wameahidi kuwa hawatawadharau Manchester United licha ya matatizo ya klabu hiyo ya Uingereza katika ligi ya nyumbani.

Paris St Germain watalenga kujipiga kifua kama miamba wa Ulaya watakapokutana na Chelsea. Timu hizo mbili zimepangwa pamoja mara moja tu mnamo mwaka wa 2004 katika awamu ya makundi ya Champions League. Chelsea ilishinda mjini Paris kabla ya kutekwa sare mjini London. Mechi za mkondo wa kwanza zitachezwa mnamo Aprili mosi na mbili huku mikondo ya pili ikichezwa April inane na tisa. Finali itakuwa mjini Lisbon mnamo Mei 24.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef