1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari wa Nairobi waanza mgomo

Shisia Wasilwa
21 Agosti 2020

Shughuli katika hospitali za umma Nairobi, Kenya zimekwama baada ya madaktari kuanza mgomo wao. Hayo yanajiri baada ya madaktari hao kutoa ilani ya siku saba kwa kile wanachokitaja kuwa ni mazingira mabovu ya kazi.

https://p.dw.com/p/3hI0c
Kenia Ärztestreik Streik
Picha: picture alliance/AP Photo/B.Curtis

Mgomo wa madaktari hao ulioanza usiku wa manane huku maambukizi ya COVID 19 yakiongezeka, unayaweka maisha ya maelfu ya wagonjwa katika hatari baada ya mazungumzo kati ya chama chao na shirika la kutoa Huduma jijini Nairobi kusambaratika.

Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari na Wafamasia nchini Kenya tawi la Nairobi Daktari Maelo Deogratious anadai kuwa madaktari wanaohudumia wagonjwa wa COVID-19 hawana bima ya afya ilhali maisha yao yamo hatarini.

Fedha zilizotolewa na rais

Rais Kenyatta alitoa shilingi bilioni tatu kwa wizara ya afya, huku sehemu ya fedha hizo ikitakiwa kutolewa kwa bima ya madaktari. Madaktari hao wanadai kuwa hawajapokea fedha hizo.

Kwa mujibu wa chama cha Madaktari na Wafamasia jijini Nairobi hawajakuwa na bima ya afya tangu Julai mosi. Ripoti iliyotolewa na madaktari hao inasema kuwa baadhi yao walioambukizwa virusi vya corona walilazimika kugharamia matibabu yao walipokuwa wanaugua.

Kenia Kenyatta National Hospital - Krankenhaus in Nairobi
Madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta Nairobi, KenyaPicha: picture-alliance/dpa/Kenyatta National Hospital

Aidha, wanadai kuwa hawajalipwa mishahara yao ya mwezi wa sita na saba. Maelo anasema kuwa jimbo la Nairobi halina eneo maalum la kuwatenga madaktari pamoja na wahudumu wengine wa afya ambao huambukizwa ugonjwa huo, wakiwahudumia wagonjwa, huku madaktari 15 wakiwa tayari wameuguwa virusi vya corona.

Mishahara yachelewa

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya Mercy Mwangangi, anasema kuwa mishahara ya madaktari ilichelewa kwa sababu ya usimamizi mpya wa jiji.

Mazungumzo kati ya madaktari na serikali yamekuwa yakifanyika kwa kipindi cha miezi sita sasa na hayajafanikiwa. Madaktari watano wamepoteza maisha yao tangu janga la virusi vya corona lilipoingia nchini Kenya, huku idadi hiyo ikihofiwa kuongezeka.

Nusu ya idadi yote ya maambukizi ya virusi vya corona imeripotiwa katika jimbo la Nairobi. Kenya imerekodi zaidi ya visa 31,000 vya ugonjwa wa COVID-19, watu 17,800 wamepona huku idadi ya waliokufa ikizidi 500.