Madaktari Ujerumani waonya usitishaji chanjo ya AstraZeneca | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Madaktari Ujerumani waonya usitishaji chanjo ya AstraZeneca

Madaktari nchini Ujerumani wameonya kuwa kusimamishwa kwa muda chanjo ya virusi vya corona ya AstraZeneca kunaweza kuchelewesha mpango wa kutoa chanjo nchini humo.

Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini Ujerumani KBV, Andreas Gassen amesema dozi milioni 17 ya chanjo kati ya milioni 60 zilizopangwa katika robo ya pili ya mwaka ni za AstraZeneca. Amesema hata usitishaji wa muda utaifanya hatua ya madaktari wa familia kutoa chanjo kuwa ngumu zaidi.

Amesema utunzaji wa chanjo nyingine ni wa gharama kubwa na mgumu zaidi, hatua inayozifanya zisiweze kutumika katika kliniki za madaktari wa kawaida. Ujerumani pamoja na Ufaransa, Italia na Uhispania ni miongoni mwa nchi wanachama za Umoja wa Ulaya ambazo zimesitisha utoaji wa chanjo ya AstraZeneca kwa madai kwamba inasababisha damu kuganda.

EMA: Chanjo haina madhara

Hata hivyo, Shirika la Usimamizi na Udhibiti wa Dawa barani Ulaya, EMA limesema chanjo hiyo ni salama na haina madhara. Aidha, Waziri wa Afya wa Uingereza, Matt Hancock amesema chanjo ya AstraZeneca ni salama na hakuna ushahidi kwamba inasababisha damu kuganda.

Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani, WHO limetangaza kuwa uchapishaji wa ripoti inayoelezea chanzo cha virusi vya corona unaweza kucheleweshwa hadi wiki ijayo. Msemaji wa WHO, Christian Lindmeier amesema ripoti hiyo haiko tayari na kwamba timu ya shirika hilo inashirikiana na maafisa wa China kuikamilisha ili kuweka mambo sawa.

Schweden Malmo | Coronavirus | AstraZeneca Impfung

Muuguzi akivuta chanjo ya AstraZeneca kwenye sindano

Nchini Uingereza takriban nusu ya idadi ya watu wazima itakuwa imepata dozi ya kwanza ya chanjo ya ugonjwa wa COVID-19 ifikapo mwishoni mwa wiki hii. Hayo yameelezwa na Waziri wa Biashara, Kwasi Kwarteng na kuongeza kuwa serikali ya Uingereza inajadiliana uwezekano wa kutoa pasi ya chanjo ya virusi vya corona.

Umoja wa Ulaya kupata dozi zaidi

Nayo Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jumanne ilitangaza kuwa imefanikiwa kupata dozi milioni 10 zaidi za chanjo ya virusi vya corona ambazo zitasambazwa na Pfizer katika kipindi cha miezi mitatu ijayo. Rais wa halmashauri hiyo, Ursula von der Leyen amesema hatua hiyo itaupa Umoja wa Ulaya kiasi cha dozi milioni 200 katika robo ya pili ya mwaka na kwamba hizo ni habari njema.

Huko barani Afrika inaelezwa kuwa nchi ya Morocco iko mbele katika mpango wa kutoa chanjo ya COVID-19 kuliko nchi yoyote ile barani humo. Hata hivyo, wahamiaji wasio na vibali sio sehemu ya mpango huo wa chanjo.

Ama kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi leo anafanya mkutano na viongozi wa majimbo ya serikali kujadiliana hatua za kuchukua kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona. Takriban visa vipya 30,000 vimetangazwa Siku ya Jumatano nchini humo, ikiwa ni idadi ya juu kabisa kurekodiwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

(DPA, AFP, Reuters, DW https://bit.ly/3bSilLG)