Madai ya rushwa dhidi ya DFB kuchunguzwa | Michezo | DW | 19.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Madai ya rushwa dhidi ya DFB kuchunguzwa

Mwendesha mashtaka wa jimbo la Hesse mjini Frankfurt atayachunguza madai ya rushwa kuhusiana na dimba la Kombe la Dunia la FIFA 2006 nchini Ujerumani

Hii ni baada ya ripoti ya jarida moja kudokeza kuwa kulikuwa na hazina ya fedha iliyotumiwa kununua kura kwa ajili ya Ujerumani kupewa kibali mwaka wa 2000 cha kuandaa dimba hilo.

Jarida la Ujerumani la Der Spiegel limeripoti siku ya Ijumaa kuwa kamati iliyoshughulikia ombi la Ujerumani kuandaa Kombe la Dunia ilitoa euro milioni 6.7 ili kununua kura katika Shirikisho la Kandanda la Kimataifa – FIFA.

Msemaji wa ofisi ya mwendesha mashtaka mjini Frakfurt Nadja Niesen amesema wameanzisha mchakato wa uangalizi ambao utaamua kama uchunguzi rasmi utaanzishwa au la.

Der Spiegel liliripoti kuwa mfuko maalum ulitengwa ambapo euro milioni 6.7 zilitolewa kama mkopo na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Adisas Robert Louis-Dreyfus kwa kamati ya Ujerumani ya ombi la kuandaa Kombe la Dunia kulipa hongo kwa maafisa wa FIFA ili kusaidia kuipa Ujerumani kibali cha kuwa mwenyeji.

Deutschland Organisationskomitee der Fußball-Weltmeisterschaft 2006

Maafisa wa kamati iliyoandaa Kombe la Dunia la FIFA 2006 nchini Ujerumani

Ripoti hiyo ilisema, ikinukuu nyaraka za ndani za Shirika la Kandanda la Ujerumani - DFB, miongoni mwa wale waliofahamu kuhusu hazina hiyo ni Franz Beckenbauer, aliyekuwa mkuu wa kamati ya maandalizi ya mwaka wa 2006, na Wolfgang Niersbach, rais wa sasa wa Shirika la Kandanda la Ujerumani ambaye alikuwa alikuwa naibu rais wa kamati hiyo.

Niersbach, Beckenbauer na DFB wamekanusha vikali madai hayo wakisema hayana msingi wakisema jarida hilo halikutoa ushahidi wowote wa kuunga mkono madao yao. Huyu hapa Niersbach "Ninapiga kabisa madai hayo. Ninawahakikishia kuwa kuhusiana na kampeni ya kutolewa kibali cha Kombe la Dunia 2006 hakukuwa na hazina zozote maalum katika DFB, Kamati yetu ya kampeni au kamati ya maandalizi. Wakati huo, mnamo Julai 2000, tulikuwa mgombea bora kabisa na tukashinda kwa kura 12 dhidi ya 11 za Ujerumani kuwa mwenyeji".

Niersbach amesema ripoti hiyo italichafua jina la DFB "Mwanzo, inaumiza sana, na tumekasirishwa kuwa tamasha hilo la kuvutia ambalo nchi yetu nzima ilisherehekea na ambalo lilikaribishwa na kila mmoja wetu kote ulimwenguni sasa lipo katika vichwa vya habari tena zaidi ya miaka tisa baadaye kwa njia kama hii. Shirikisho letu la DFB limesema kuwa lazima tujibu maswali yote ya wazi na kwa pamoja kutoa ufafanuzi. Tunafahamu kuwa tunapaswa kuueleza umma, mashabiki wa kandanda la Ujerumani".

Shirikisho la kandanda la kimataifa – FIFA lilitumbukia mnamo mwezi Mei katika mgogoro mkubwa zaidi tangu lilipoanzishwa miaka 111 iliyopota, wakati maafisa wa kandanda 14 na maafisa wa shughuli za mauzo michezoni walishtakiwa na Marekani kuhsuu madai ya rushwa, kusafisha fedha na mitandao ya ulaghai wa fedha kupitia malipo ya kiasi cha zaidi ya dola milioni 150

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu