Mada mbili zimegubika magazeti ya leo nchini Ujerumani | Magazetini | DW | 06.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Mada mbili zimegubika magazeti ya leo nchini Ujerumani

ETA watangaza kubeba upya silaha na mkutano wa kilele wa G8 mjini Heiligendamm

ETA waahidi kubeba upya silaha na matarajio ya mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kwa viwanda G-8 mjini Heiligendamm ndizo mada mbili zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.Tuanzie ng’ambo lakini.Baada ya wapiganaji wa chini kwa chini wa ETA kusema wanavunja makubaliano ya kuweka chini silaha,waziri mkuu wa Hispania José Luis Zapatero amewatolea mwito wananchi wasimame kidete dhidi ya magaidi.Gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG linaandika:

Tangazo la ETA la kuanzisha upya mapigano ni pigo kubwa kwa waziri mkuu jasiri wa Hispania José Luis Zapatero.Tangu mwanzo aliahidi kuendeleza mazungumzo tete pamoja na ETA ,akitaraji pengine angefanikiwa kufikia makubaliano ya amani sawa na yale yaliyofikiwa na Tony Blair huko la Ireland ya kaskazini.Lakini nia njema ya kisiasa haikumsaidia Zapatero.Hata uamuzi uliozusha mabishano wa kupunguza makali ya kifungo dhidi ya mwanaharakati mashuhuri wa ETA Juana de Chaos haukusaidia kitu.Hata kuruhusiwa kwa kadiri fulani chama marufuku cha Batasuna kiwaakilishwe katika chaguzi za hivi karibuni za mabaraza ya miji-hawajashukuria.”

Gazeti la NEUE WESTFÄLISCHE la mjini Bielefeld linaamini:

Matumaini ya amani yametoweka moja kwa moja hivi sasa nchini Hispania.Tangazo jipya la vita lililotolewa na magaidi wa Basque-ETA linaifanya nchi hiyo inayopendwa na watalii ihofie wimbi jipya la matumizi ya nguvu.ETA wanang’ang’ania madai yale yale yasiyotekelezeka:yaani kutengwa eneo lote la Basque tangu lile la Hispania mpaka lile lililoko Ufaransa na kujipatia uhuru wake.Madai hayo kamwe hayawezi kukubaliwa na serikali ya mjini Madrid.

Gazeti la mjini Berlin-Die BERLINER ZEITUNG linajiuliza kama amani kweli inaweza kupatikana hivi sasa.Gazeti linaendelea kuandika:

Ajuae Mungu lini utaratibu wa amani utaanza upya nchini Hispania.Kwamba hawana njia nyengine isaipokua kufikia amani,hiyo hakuna asiyejua.Kwasababu mvutano kuhusu haki ya kujiamulia wenyewe mambo yao wakaazi wa Basque- unaotumiwa tangu miongo kadhaa na ETA,ni wa kisiasa na unabidi pia upatiwe ufumbuzi wa kisiasa.Ni hadaa waaminivyo wanaharakati wa Etarras kwamba mabomu yanaweza kufungua njia ya kujipatia uhuru,sawa na vile wanavyoamini wahispania wengi eti polisi na vyombo vya sheria pekee watatosha kuwavunja nguvu wanaharakati wanaopigania kujitenga jimbo la Basque.“

Mada ya pili kubwa magazetini hii leo ni kuhusu mkutano wa viongozi wa G-8 mjini Heiligendamm.Gazeti la MITTELDEUTSCHE ZEITUNG la mjini Halle linazungumzia juu ya hatua za usalama na kuendelea kuandika:

„Risasi za mpira dhidi ya wafanya fujo,anadai kwa mfano Sebastian Edathy wa chama cha Social Democratic.Kutoka vyama ndugu vya CDU/CSU sauti zinazidi kupazwa kutaka vikosi maalum vya GSG 9 vilinde usalama.Kipi chengine?Tuache mzaha sasa.Mjadala uliozuka kutokana na hatua kali za usalama hauna maana.Waliojeruhiwa zaidi,machafuko yaliporipuka mjini Rostock ni polisi na wale waliokua wakiandamana kwa amani.Wote wawili wangefanya la maana kutuepushia mapendekezo kama hayo.“

Gazeti la Die Welt linaandika:

„Kama katika mikutano iliyopita ya G-8,na safari hii pia viongozi wa taifa na serikali wameorodhesha matatizo yote ya dunia katika ajenda yao ya mazungumzo na kubainisha wakati huo huo hakuna chochote kitakachoamuliwa.Hakuna yeyote anaeweza kuyajadili kwa dhati masuala yote tete kwa muda mfupi kama huo..Masuala mengi,mfano yale ya kibiashara, ingekua bora yangejadiliwa katika duru nyengine.“

 • Tarehe 06.06.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSm
 • Tarehe 06.06.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSm
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com