1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron awaomba wapinzani kuepusha mkwamo wa kisiasa

Lilian Mtono
23 Juni 2022

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema makundi ya upinzani yameonyesha utayari wa kushirikiana naye katika masuala muhimu baada ya muungano wake wa kisiasa wa Ensemble kupoteza wingi wa viti katika bunge la kitaifa.

https://p.dw.com/p/4D5xQ
Frankreich Ansprache vom Präsident Macron im Fernsehen
Picha: Ludovic Marin/AFP

Rais Emmanuel Macron tayari amekutana na viongozi wa makundi hayo kwa lengo la kusaka uungwaji mkono wa kutosha bungeni, lakini pia kumaliza kile kinachoonekana ni mkwamo wa kisiasa nchini Ufaransa.

Rais Emmanuel Macron amesema kwenye hotuba yake kupitia televisheni jana Jumatano kwamba Ufaransa inahitaji mageuzi makubwa na ili hayo yafikiwe ni lazima kuwepo na maelewano.

"Ili kufanya kwa maslahi yako na ya taifa, inatulazimu tujifunze jinsi ya kutawala kwa njia tofauti na kujenga maelewano mapya na makundi ya kisiasa ambayo yanaunda bunge jipya kupitia mazungumzo, kusikiliza, na kwa heshima," alisema Macron.

Hiyo ilikuwa ni hotuba ya kwanza kwa taifa tangu muungano wake wa Ensemble kupoteza wingi wa viti bungeni katika uchaguzi uliofanyia Jumapili iliyopita.

Soma Zaidi:Macron akosa wingi wa kutosha bungeni 

Emmanuel Macron und Christian Jacob
Rais Emmanuel Macron akiwa na kiongozi wa chama cha upinzani cha LR, Christian Job baada ya mazungumzo jana JumannePicha: Mohammed Badra/AFP /Getty Images

Baada ya kukutana na wawakilisha wa upinzani baada ya uchaguzi huo, Macron amesema pande hizo nyingine za kisiasa zilionyesha utayari wa kujadiliana masuala mazito ikiwa ni pamoja na gharama za maisha, ajira, masuala ya nishati, mabadiliko ya tabianchi na afya.

Kulingana na Macron, sheria ya dharura inayolenga kukabiliana na mfumuko wa bei na ongezeko la gharama za nishati utawasilishwa bungeni katika majira haya ya joto. Amesisistiza kwamba gharama za mabadiliko ya kisheria hazitalipiwa na kodi kubwa ama kwa kuingia kwenye deni jipya.

Macron aupa muda upinzani kufanya maamuzi, akiri mpasuko wa kitaifa.

Rais Macron pia amevitolea mwito vyama vya upinzani kufafanua kwa uwazi ni kwa kiasi gani watakuwa tayari kuunga mkono hatua hizo. na kuwapa masaa 48 yajayo kutangaza msimamo wao.

Alisema "Tunapaswa kufafanua katika siku zijazo mwelekeo wa kiuwajibikaji na ushirikiano ambao makundi ya upinzani bungeni yapo tayari kuuchukua. Ama kuingia kwenye muungano na serikali na kusonga mbele, au kujitolea kupitisha baadhi tu ya miswada, kujadili  bajeti yetu.... na Ili kusonga mbele, ni juu ya makundi haya kueeza wazi ni kwa kiasi gani wako tayari."

Kiongozi huyo aidha amekiri mipasuko na migawanyiko mikubwa nchini humo, iliyojidhihirisha wazi kupitia matokeo wa uchaguzi huo wa bunge.

Muungano wa Macron, bado unasalia mkubwa ukiwa na viti 245 kati ya 577 katika bunge la kitaifa, lakini hata hivyo hauna wingi unaotakiwa ambao umekuwa nao katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Mwaka 2017, muungano huo wa Macron uipata viti 308 vya bunge.

Sikiliza Zaidi:

Mwangaza wa Ulaya: Macron na serikali isiyo na nguvu bungeni

Mashirika: DW