1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron aandaa mkutano wa kilele kuhusu Afrika

6 Oktoba 2021

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa atakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele juu ya Afrika siku ya Ijumaa, ingawa hautahudhuriwa na viongozi wengine wa serikali.

https://p.dw.com/p/41LnL
Frankreich | G5 Gipfel | Präsident Emmanuel Macron
Picha: Blondet Eliot/ABACA/picture alliance

Katika mkutano huo utakaofanyika katika mji wa kusini mwa Ufaransa wa Montpellier, Rais Macron atakutana na wafanyabiashara vijana, wasanii na wanamichezo, akiazimia kurekebisha mahusiano kati ya nchi yake na bara la Afrika.

Watu 3,000 wakiwemo vijana 1,000 wanatazamiwa kuhudhuria majadiliano hayo juu ya masuala ya kiuchumi, kitamaduni na kisiasa. Ofisi ya rais huyo wa Ufaransa imesema dhamira ya mkutano huo ni kusikiliza maneno ya vijana wa Kiafrika na kuachana na mifumo na miundo ya zamani.

 Mkutano huo unakuja katika kipindi tete kati ya Ufaransa na makoloni yake mengi yanayozungumza Kifaransa barani Afrika, baada ya uamuzi wa kuwataka raia kutoka Algeria, Morocco na Tunisia kuomba vibali vya kuingia Ufaransa. Algeria ilimuita balozi wake nyumbani baada ya Macron kusema nchi hiyo inaongozwa na "mfumo wa siasa za kijeshi", ambapo Mali imekasirishwa na majibu ya Ufaransa kuhusu mipango ya nchi hiyo ya ukanda wa Sahel kutaka kuleta mamluki wa Kirusi kwenye vita dhidi ya wapiganaji wa siasa kali.

Macron atakuwa anajadiliana na jopo la vijana baada ya miezi ya mazungumzo

Muundo mpya wa mkutano huo unaonyesha kufadhaika kwa Ufaransa, ambayo imefanya mikutano na viongozi wa Kiafrika tangu 1973, pamoja na uongozi wa kisiasa wa nchi zingine.

Tschad Präsident Idriss Deby
Emmanuel Macron akiwa na viongozi wa baadhi ya nchi za AfrikaPicha: Guillaume Horcajuelo/POOL/AFP/Getty Images

Macron yuko mbioni kujadiliana na jopo la vijana walioteuliwa baada ya miezi ya mazungumzo ilioongozwa na msomi kutoka Cameroon, Achille Mbembe ambaye ndiye anayesimamia maandalizi ya mkutano huo.

Afisa kwenye Ikulu ya rais Macron ambaye hakutaka kutajwa jina amesema masuala ambayo inayosababisha kero yatakuwa mezani, akiongoza kuwa muktadha wa kisiasa hivi sasa wafanya mazungumzo kuwa nyeti.

Maafisa wa Ufaransa wanaahidi mapendekezo halisi kutoka kwa ripoti ambayo Mbembe atawasilisha kwa Macron.

Emmanuel Macron aliapa katika hotuba yake ya Novemba 2017 mjini Ouagadougou, nchini Burkina faso, kuchukuwa njia mpya kuhusu bara la Afrika,ambapo Ufaransa haitawaambia Waafrika tena nini cha kufanya.

Pia, Macron ameweka hatua ya kufikia Afrika inayozungumza Kiingereza ili kujenga nguvu zaidi mbali na milki ya zamani ya Ufaransa barani humo.

Leo  Alhamisi, Macron atakutana jijini Paris na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, ambaye bado ni mtu mwenye ushawishi mkubwa barani. Tangu hotuba ya 2017, kazi za sanaa na za kitamaduni zilizoporwa kutoka Benin zimerejeshwa na Ufaransa imetangaza mipango ya kurekebisha FrancCFA, sarafu inayotumiwa katika nchi kadhaa barani Afrika lakini imetengenezwa na kuhifadhiwa na Ufaransa.

Mkutano huu unaweza kuleta uhusiano mpya kati ya Ufaransa na Afrika

Wakati huo huo, ripoti iliyopewa dhamana na Macron ilikubali "majukumu makubwa" ya Ufaransa juu ya mauaji ya kimbari ya 1994 huko Rwanda, suala ambalo lilikuwa sumu katika mahusiano kati ya Paris na Kigali.

Amadou Sadjo Barry,mwanafalsafa wa Canada mwenyeasili ya Guinea amesema tangu hotuba ya Macron huko Ouagadougou, mistari imehamia kinadharia, kumekuwa na ishara muhimu. Lakini kwa suala la sera za kigeni, hatuwezi kuzungumzia mabadiliko makubwa,alisema .

Ufaransa inaendelea kuvumilia serikali zisizo za kidemokrasia, ikikubali haraka kukabidhiwa madaraka kutoka kwa rais wa Chad Idriss Deby Itno kwa mtoto wake mnamo Aprili.

Tschad | Mahamat Idriss Déby, Präsident des Übergangs-Militärrates (CMT)
Idriss DebyPicha: Christophe Petit Tesson/REUTERS

Wakati muundo wa mkutano wa Montpellier unaweza kusaidia kuleta maisha mapya katika uhusiano wa Ufaransa na Afrika, Barry alielezea mkutano huo kama "ushindi wa mfano kwa Afrika".

Sadjo Barry alihoji kwa nini bado mustakabali wa binadamu, siasa na uchumi wa bara la Afrika unajadiliwa nchini Ufaransa? Kwa nini serikali za Kiafrika hazisikilizi kero za watu wao?