Machafuko kisiwani Madagascar | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Machafuko kisiwani Madagascar

Upande wea upinzani kisiwani Madagascar walalamika dhidi ya serikali

Rais wa Madagascar Marc Ravalomanana

Rais wa Madagascar Marc Ravalomanana
Meya wa mji mkuu wa Madagascar,Antananarivo,Andry RAJOELINA,mpinzani mkubwa wa rais RAVALOMANANA amezidisha makali ya mvutano dhidi ya serikali kwa kuwakusanya maelfu ya wafuasi wake hii leo katika maandamano yaliyogeuka kua matumizi ya nguvu.


Jengo la Radio ya taifa Radio National Malgache-RNM iliyoko katika eneo la kati la mji mkuu Antananarivo limevamia,na baadae kutiwa moto.


Wafanyafujo hao ni sehemu ya maelfu ya wafuasi wa upande wa upinzani waliokusanyika leo asubuhi katika uwanja wa May 13-kitovu cha malalamiko ya wabuki,wakijibu mwito wa mgomo jumla uliotolewa ijumaa iliyopita na Meya Andry Rajoelina anaekosoa kile anachokiita "uimla unaoendelea Madagascar."


Usafiri katika mji mkuu wa Madagascar umeparaganyika kutokana na izuwizi vilivyowekwa majiani.


Licha ya onyo la serikali,meya wa Antananarivo Andry Rajoelina amemlaumu rais Marc Ravalomanana na serikali yake anayoitaka kua ni ya kimabavu na kusema tunanukuu:"Madaraka yanamilikiwa na umma.Unaweza kunyakua madaraka hayo.Kila saa inapopita,serikali inadhihirisha uimla" mwisho wa kumnukuu meya huyo kijana wa miaka 34 aliyewataka wafuasi wa upande wa upinzani wateremke tena majiani kesho.


Andry Rajoelina,ambae pia ni mfanyabiashara amekua akizozana na utawala wa rais Ravalomanana tangu alipochaguliwa kua meya wa Antananarivo December mwaka 2007.


Mzozano wao umezidi makali baada ya serikali kuamua kukifunga kituo cha televisheni cha kibinafsi Viva,december 13 mwaka jana-baada ya kituo hicho kufanya mahojiano pamoja na rais wa zamani Didier Ratsiraka anaeishi uhamishoni nchini Ufaransa tangu mwaka 2002.


Rais Marc Ravalomanana amefupisha ziara yake nchi za nje na kurejea nyumbani jana,akisema "anataka kurejesha nidhamu na kuihami Jamhuri".


"Mwito wa kutoheshimu amri ya serikali uliotolewa na meya wa Antananarivo ni sawa na njama ya mapinduzi na unavuruga maadili ya kikatiba."Amesema hayo rais Marc Ravalomanana katika taarifa yake .


Ikiwa chanzo cha mtafaruku ni kufungwa kituo cha televisheni ya kibinafsi ya Viva,meya Rajoelina anakosoa pia ukosefu wa haki ya mtu kutoa maoni yake na ukosefu wa demokrasia katika kisiwa hicho kikuu pamoja na kunyakuliwa ardhi za wabuki kwa masilahi ya mradi mkubwa wa kilimo unaosimamiwa na shirika la Korea ya kusini-Daewoo.


Upande wa upinzani kisiwani Madagascar unakosowa pia makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya serikali na mashirika ya kigeni ,ikihusika pia sekta ya maadini katika wakati ambapo nchi hiyo inazidi kudidimia katika bahari ya umaskini.
 • Tarehe 26.01.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GgWa
 • Tarehe 26.01.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GgWa
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com