Mabishano baina ya Marekani na Ujerumani kuhusu Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mabishano baina ya Marekani na Ujerumani kuhusu Afghanistan

Watetezi watatu wanaotaka kuchukuwa nafasi ya sasa ya Rais wa Marekani wanatafautiana katika masuala kadhaa ya programu za kisiasa.

Seneta Barack Obama, anayewania utetezi wa urais wa Marekani kwa niaba ya Chama cha Democratic

Seneta Barack Obama, anayewania utetezi wa urais wa Marekani kwa niaba ya Chama cha Democratic

Lakini katika suala moja wote wanakubaliana, nalo ni kwamba nchi za Ulaya, na hasa Ujerumani, zinafaa zipeleke wanajeshi zaidi hadi Afghanistan.

Mvutano ndani ya jumuiya ya kujihami ya nchi za Magharibi, NATO, hasa baina ya Marekani na Ujerumani, juu ya namna ya kugawana mzigo wa kuendesha vita dhidi ya Wataliban na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida nchini Afghanistan, ulijidhihirisha kichinichini na kuzungumziwa kindani ndani wakati wa ziara ya katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Jaap de Hoop Scheffer, mjini Washington wiki iliopita. Bwana Scheffer alizungumzia kwamba haifai nchi wanachama wa umoja huo kutupiana lawama, huku akisema kwamba yahitaji kuweko mashikamano makubwa zaidi baina ya nchi wanachama. Suala hilo pia litatwama katika mahusiano baina ya nchi za Ulaya na Marekani, bila ya kujali nani ataingia Ikulu ya Marekani na kuchukuwa mahala pa George Bush.

Wakati alipokutana na katibu mkuu wa Jumuiya ya NATO, Jaap de Hoop Scheffer, katika Ikulu ya Washington, Rais George Bush alisema takwa la muda mrefu la Marekani na lililo wazi ni kwamba:

"Lazima tuhakikishe kwamba NATO inabakia kuwa jumuiya muhimu ambayo inailetea dunia usalama na amani. Tunahisi tunawajibika kuchangia katika shughuli za NATO katika Afghanistan."

Sio zote, lakini Marekani hairidhiki na nchi nyingi za NATO, kama vile Ujerumani, namna zinavotenda kuhusu suala hilo. Na jambo hilo limeelezewa kinaga ubaga ndani ya barua alioiandika waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, kwa waziri mwenzake wa Ujerumani, Franz Josef Jung, ambapo aliitaka Ujerumani itume wanajeshi zaidi hadi Afghanistan na iwaweke kusini mwa nchi hiyo.

Lakini kwa wakati huu lugha inayotumiwa sio kali mno, lakini bado Marekani inashikilia juu ya takwa lake, na bila ya shaka takwa hilo pia litakaririwa baada ya uchaguzi wa urais wa huko Marekani, mwezi Novemba mwaka huu. Na sasa pia mtu wa tatu katik lile kundi la watu ambao huenda wakawa warithi wa George Bush katika Ikulu ya Washington, hajatetereka hata kidogo katika msimamo wake. Naye ni Barack Obama wa kutoka Chama cha Democratic ambaye alitangaza kwamba pindi atachaguliwa kuwa rais basi atavimaliza kwa haraka kama iwezekanavyo vita vya Iraq, na badala yake kuishughulikia Afghanistan. Alipokuwa yuko katika ndege juu ya anga ya mkoa wa Texas katika kampeni yake ya uchaguzi, Barack Obama alisema anatarajia nchi za Ulaya zitachangia zaidi katika vita vya Afghanistan:

"Tunahitaji kuungwa mkono zaidi kutoka nchi za Ulaya na kuweko vizingiti vichache zaidi katika kuweka majeshi yao huko. Haiwezekani kwamba Marekani na Uengereza ndio zifanye kazi chafu."

Kwa hivyo ni wazi. Pia Barack Obama ambaye huko Marekani na katika nchi za kigeni anatukuzwa, pindi atakuwa rais hatokuwa malaika wa amani. Atakuwa sawa na mtu mwengine anayetarajiwa kuwa mtetezi wa urais kutoka chama chake cha Democratic, naye ni Bibi Hilary Clinton. Bibi huyo pindi atakuwa rais atavikomeshe vita katika Iraq na pia atataka upatikane ushindi katika vita vya Afghanistan. Tangu sasa anawaza juu ya jambo hilo:

"tutafanya kile tunachoweza kufkiikia, nacho ni kuweko majeshi mengi ya NATO katika Afghanistan."

Profesa Julius Nyangoro wa Chuo Kikuu cha Mkoa wa Carolina ya Kaskazini huko Marekani hajagundua tafauti yeyote kati ya watetezi hao watau kuhusu vita vya Afghanistan:

Kwa hivyo itegemewe kwamba nchi za Ulaya, ikiwemo Ujerumani, zitawekewa mbinyo, na jambo hilo litawezekana zaidi pindi Bibi Hilary Clinton atakuwa rais. Pia John MCcain, ambaye karibu ni hakika atakuwa mtetezi wa Chama cha Republican, anaunga mkono jambo hilo. Yeye anataka majeshi ya Marekani yaendelee kupigana huko Iraq na pia Afghanistan, na yeye anajuwa wazi kwamba jambo hilo halitawezekana bila ya msaada mkubwa wa kutoka nchi rafiki.

"Bahati mbaya baadhi ya nchi hizo rafiki zimeweka vizingiti vikubwa katika kupeleka wanajeshi wao huko Afghanistan, kwamba yasifanye operesheni zao kusini mwa Afghanistan au yasifanye harakati wakati wa usiku. Lazima tuzifanye nchi hizo zirejee katika mchezo, lazima zitusaidie zaidi kuliko zilivokuwa zikifanya hapo kabla."

Jambo moja limewekwa wazi na Seneta Barack Obama, nalo ni kwamba ushirikiano baina ya Marekani na nchi za Ulaya hautakiwi kuwa njia inayoelekea upande mmoja tu.:

"Ni muhimu kwamba tuombe zaidi kutoka kwa washirika wetu wa Ulaya, lakini pia lazima tutilie maanani kikweli fikra zao, na hasa linapokuja suala la Iraq. Na sasa lazima mimi nikae pamoja nao na kuya-chambua mambo."

Kwa baadhi ya Wamarekani na watu wa nchi za Ulaya, vita vya Iraq na Afghanistan ni uchafu na matope ambayo kwamba serekali ya Marekani imeingia ndani yake, na kuna baadhi ya watu wa Ulaya kwanini na wao wapakazwe uchafu huo? Tena Profesa Julius Nyangoro wa Chuo Kikuu cha Carolina ya Kaskazini huko Marekani:

Bila ya shaka itarajiwe kwamba kutakuweko na mitikisiko ya kisiasa katika uhusiano baina ya Marekani na Ulaya.

 • Tarehe 04.03.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DHrK
 • Tarehe 04.03.2008
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DHrK
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com