Mabingwa tena ni Misri | Michezo | DW | 01.02.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Mabingwa tena ni Misri

Kombe la Afrika laenda Cairo mara ya 7.

Shabiki wa mafiraouni (Misri) akipiga zumari la ushindi.

Shabiki wa mafiraouni (Misri) akipiga zumari la ushindi.

MISRI MABINGWA X 3 MFULULIZO:

Misri, imetawazwa mabingwa wa Afrika kwa mara ya 3 mfululizo na mara ya 7 kwa jumla. Je, kwanini chipukizi wa Black Stars (Ghana) hawakufua dafu mbele ya mafiraouni na ilikuaje timu zote 5 zitakazowakilisha Afrika katika Kombe lijalo la dunia Afrika Kusini Juni hii, zimesshindwa kufua dafu mbele ya Misri ? Katika Bundesliga-Bayer Leverkusen, yaendelea kuun'gania usukani kileleni na FC Cologne nayo yatoroka na pointi 3 nyengine kutoka Frankfurt.

Misri ,mabingwa waliondoka jana Luanda na taji lao la 7 na la 3 mfululizo la Kombe la Afrika la mataifa na kumtawaza kitini jogoo wao mpya "Gedo Ngay" anaefuata nyayo za "Bibo El-Khatib, Hossam Hassan,Mohamed Aboutrika na Mohamed Zedan wa bundesliga. Gedo, asiejulikana nje ya Misri kabla Kombe hili la Afrika kwa kutia mabao kila mechi aliocheza Angola, Gedo, ametia jumla ya mabao 5-muhimu kabisa ni lile la jana lililowatawaza mafiraouni kitini kama "masultani" wa dimba la afrika na kocha wao mzee Hassan Shehata. Ni Gedo aliepasiana maridadi kabisa na Mohamed Zedani na kuvunja tumbuu ya lango la Black Stars- Ghana mnamo dakika ya 85 ya mchezo na kulirudisha Kombe nyumbani cairo, mako makuu ya shirikisho la dimba la Afrika (CAF).

TIMU 5 ZA KOMBE LA DUNIA:

Isipokuwa Black Stars Ghana,hakuna timu nyengine kati ya 5 zinazokwenda Afrika kusini kwa kombe lijalo la dunia,iliondoka Angola na heshima yake.Ghana inaweza kwenda Afrika kusini ikiwa na matumaini ya kupepea bendera ya Afrika baada ya kutamba hadi finali licha ya kuwa mastadi wake kadhaa pamoja na Michael Essien wameumia na hawakuweza kucheza.

Ghana inafungua dimba la kombe la dunia kwa mpambano na Serbia, Juni 13, kabla kutimiza miadi yake na Ujerumani na halafu Australia.Si ajabu basi shabiki mmoja kusema ulimwengu unapasa kuikodolea macho Ghana.

"Haya ni mashindano ya kwanza kabisa kwa chipukizi wa Ghana na tumejifunza mengi kwa maandalio ya kombe lijalo la dunia tena kutoka kila mechi na siku moja tutavaa taji." Alisema shabiki huyo wa Black Stars".

Nigeria, iliitoa Algeria kwa bao 1:0 na kutwaa nafasi ya 3 jumamosi.Lakini, nani atakataa kwamba, Super eagles hawakunawiri katika kombe hili la Afrika.Walitokwa na jasho kabla kuzima vishindo vya Chipolopolo-Zambia,lakini mbele ya jirani zao Ghana, walishindwa kufua dafu.

Sasa hatima ya kocha wao Shuabi Amodu, imewekewa kikao maalumu Ijumaa hii ijayo na shirikisho la dimba la Nigeria.Shoka linameta-meta kumfyeka kabla Kombe la dunia.

Algeria,ilianza vibaya ilipoteleza mbele ya chipukizi Malawi ilipochapwa mabao 3:0,lakini iliporudi tena uwanjani ilikua taabu kuitambua Algeria.Waalgeria waliwapioga kumbo Tembo wa Ivory Coast na kuwatoa katika robo-finali na kuweka miadi na mahasimu wao mafiraouni-Misri.Katika marudio ya vita vyao vya kufuzu kwa Kombe la dunia, mafiraouni wakalipiza kisasi kwa kuipiga kumbo Algeria kwa mabao 4:0.

Ivory Coast,timu nyengine inayokwenda kucheza kombe la dunia,iliwasili Angola, ikipigiwa upatu ndio timu hasa ya kuwavua taji mafiraouni.Tembo waliacha uongozi wao wa mabao 2:1 dhidi ya Algeria kugeuka pigo la dakika ya mwisho la mabao 3-2. Uzembe wao uliwarudisha Tembo msituni na mapema.

Simba wa nyika-Kameroun, walifika robo-finali tu walikotimuliwa kwa mabao 3-1 na mafiraouni, Misri.Hatashivyo, Simba wa nyika wanadai wamejifunza darasa lao huko Angola.

Darasa lakini, hawajajifunza pekee yao kama asemavyo shabiki huyu: anaesema:

"Dimba mtu hujifunza huku akiendelea na kuna mema yaliojitokeza katika Kombe la Afrika na ambayo mtu aweza kuyatumia kama msingi wa maandalio ya kombe lijalo la dunia."

Huko Uingereza, ilikua changamoto kati ya Manchester United na Arsenal na mjini Luanda, finali ya kombe la Afrika kati ya Misri na Ghana:Mashabiki wa Kenya walipata taabu kuamua waangalie dimba lipi.

Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani,Bayer Leverkusen, iliwaambia mabingwa mara kadhaa Bayern Munich, walioparamia kileleni hapo Jumamosi kwamba, "alie juu ,mgoje chini."Leverkusen wakaaikandika jana Freiburg mabao 3-1 na kuunyakua tena uongozi wa Bundesliga.

Hata Schalke, inayonyatia kutoka nafasi ya 3, ilitoa salamu hizo hizo kwa Bayern Munich ilioitandika Mainzi, Jumamosi mabao 3-0. Schalke, ikitamba na Kevin Kuranyi na kocha wao Felix Magath,iliikomoa Hoffenheim kwa mabao 2:0.Baadae kocha wa Schalke alietawaza Wolfsburg msimu uliopita mabingwa, alisema:

"Shabaha yangu ni kumaliza nafasi ya 6 au 7 ya ngazi ya Ligi.Kwahivyo, inatupasa kujitahidi zaidi kujiimarisha kileleni ili tusije tukaangukia nje ya nafasi ya 6."

FC Cologne, baada ya kuwatimua mabingwa Wolfsburg wiki iliopita, waliongeza jana pointi 3 nyengine huko Frankfurt,walipoizaba Frankfurt mabao 2:1 ingawa bao lao la pili lilikuwa la bahati.

Kocha wao Saldo aliungama:

"Nadhani tulitamba zaidi kuliko wenzetu na hivyo ingawa kwa bahati tulistahiki ushindi."

Mwandishi:Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman