1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabalozi wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wazuru Darfur

Kalyango Siraj5 Juni 2008

Luis Moreno Ocampo atoa ripoti kwa UM kuhusu Darfur

https://p.dw.com/p/EELV
Mkuu wa tume ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuhusu Darfur, Rodolphe Adada, akizungumza na waandhishi habari wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya Darfur ya tume ya pamoja katika mji wa El Fasher, Sudan mwaka jana .Picha: AP

Mabalozi kutoka baraza la Usalama la Umoja wa mataifa leo alhamisi wamezuru eneo la Sudan la Darfur ili kujionea wenyewe hali ilivyo kwa sasa kutokana na mgogoro ambao umedumu miaka mitano na vilevile kuona jinsi wanavyoweza kusaidia kuumaliza.

Ziara ya mabalozi hao 15, katika eneo tete la Darfur lilioko magharibi mwa Sudan,imekuja huku mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai Luis Moreno-Ocampo akiwa nae anajitayarisha kuwasilisha ripoti kwa baraza la usalama la umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo itafafanua nia yake ya kutaka kuwaandama maafisa wandamizi wa serikali ya Khartoum ambao wanahusika na uhalifu wa kivita katika eneo la Darfur. Hata hivyo hatua ya mwendesha mashataka imeikasirisha serikali ya Sudan.

Kuhusu safari ya mabalozi kwenda Darfur,wajumbe hao walifikia mji wa El Fasher,ambao ni mji mkuu wa jimbo la Darfur kaskazini kuliko makao makuu ya kikosi cha kulinda amani Darfur cha mseto wa majeshi wa Umoja wa Mataifa pamoja na ya Umoja wa Afrika kinachoitwa kwa kifupi UNAMID.

Ujumbe huo ukiondoka huko utarejea Khartoum na kufanya mazungumzo na kiongozi wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir.

Kiongozi wa Sudan amekuwa akishinikizwa kukubali kutumwa kwa kikosi cha UNAMID kinachojumulisha wanajeshi na polisi elf 26 katika eneo la Darfur.Kwa sasa kuna askari 9,000 wa kulinda amani katika eneo ambalo ukubwa wake unalinganishwa na taifa la Ufaransa.

Mjumbe maalum anaejumulisha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika,akiishughulikia Darfur Rodolphe Adada, amewaambia maripota kuwa kuna haja ya kuwa na wanajeshi zaidi,na kuonya kuwa ikiwa watasubiri zaidi,wanaweza kupoteza imani miongoni mwa wananchi kitu ambacho ni silaha muhimu katika kazi hiyo.

Utawala wa Khartoum ulisema jana kuwa vikosi vya Thailand na Nepal vinaweza vikatumwa Darfur baada tu ya kutumwa pia askari wa Misri na Ethiopia.

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa John Sawers amewaambia waandishi habari kuwa kuna mazingira bora sasa ya ushirikiano kati ya Sudan na kikosi cha mseto wa Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika.

Lakini ameongeza kuwa baraza la usalama litatoa orodha kadhaa ya yale yanayohitaji kuboreshwa zaidi.Orodha hiyo wataitoa kwa maafisa wa serikali ya Sudan.

Kwa mda huohuo,Sudan imemlaumu mwendesha mashataka wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai kwa kile ilichokiita kuvuruga mipango ya amani katika eneo la Darfur. Moreno Ocampo anataka kuwaandama maafisa wa Sudan wanaoshtumiwa kwa uhalifu wa kivita katika Darfur.

Anataka kukamatwa kwa washukiwa wawili wa Sudan ambao wanatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kijinai. Maafisa wa Khartoum wamesema hawatashirikiana na mahakama hiyo.