1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabaki ya ndege ya Misri yapatikana

John Juma19 Mei 2016

Jeshi la Misri limepata mabaki ya ndege hiyo kilomita 290 kaskazini ya Cairo. Baadhi ya mizigo ya abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo pia imepatikana. Kinachotafutwa sasa ni kisanduku cha mawasiliano au "black box"

https://p.dw.com/p/1IqQg
Ndege ya Misri.
Ndege ya Misri.Picha: picture-alliance/dpa/K.Elfiqi

Juhudi za kutafuta kisanduku kinachorekodi mawasiliano au Black box cha ndege hiyo inaendelea. Ndege hiyo ya Misri ilianguka usiku wa kuamkia Alhamisi ikiwa na abiria 66 miongoni mwao wahudumu wa ndege hiyo. Shughuli ya kutafuta mabaki yake ilianza jana na sasa imezaa matunda baada ya kupatikana kwa mabaki ya ndege hiyo kilomita 290 kutoka Cairo pamoja na baadhi ya mizigo ya abiria waliokuwemo ndani yake pia imepatikana.

Waziri wa safari za anga nchini Misri amesema uwezekano kuwa ndege hiyo ilishambuliwa kigaidi angani ni mkubwa kuliko hitilafu za mitambo kusababisha kutoweka kwake.

Waziri mkuu wa Misri Sherif Ismail alipoulizwa uwezekano wa njama ya kigaidi katika mkasa huo amejibu kuwa hawapuuzilii sababu yoyote inayoweza kukisiwa kusababisha ndege hiyo kuanguka.

Sababu ya kutoweka ni gani?

Vikosi vya usalama vya Misri vikishirikiana na vikosi kutoka Ugiriki vinaendeleza shughuli za kutafuta mabaki zaidi katika bahari ya Mediterania.

Waziri wa ulinzi nchini Ugiriki Panos Kammenos amesema ndege hiyo aina ya Airbus ilifanya mizunguko miwili ya ghafla angani na kushuka ghafla kutoka futi 37,000 hadi futi 15,000 angani, kisha ikatoweka kutoka kwenye mtambo wao wa rada.

Ndege ya Misri.
Ndege ya Misri.Picha: Imago/Tass/D. Osipov

Awali rais wa Ufaransa Francois Hollande alikariri kuwa uchunguzi kamili unahitajika kubaini mkasa huo umesababishwa na nini.

Maafisa nchini Misri wamesema kuwa ndege ya taifa hilo iliyokuwa ikisafiri kutoka Paris Ufaransa kuelekea Cairo imetoweka na huenda imeanguka katika bahari ya Mediterrania. Ndege hiyo ya shirika la EgyptAir ilikuwa na jumla ya watu 66 miongoni mwao wahudumu wa ndege hiyo. Shughuli za kutafuta mabaki ya ndege na manusura imeanzishwa.

Ndege hiyo ilitoweka na kutoonekana tena kwenye mtambo wa rada dakika 45 kabla ya muda kamili ambao ilitarajiwa kutua katika uwanja wa ndege wa Cairo. Maafisa nchini Misri wanasema ndege hiyo ilianguka mwendo wa saa nane usiku majira ya Misri, jumla ya saa tatu na nusu tangu kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris. Hii ni muda mfupi baada ya ndege hiyo kutoweka na kutoonekana tena kwenye mtambo wa rada maili kumi ndani ya anga ya Misri.

Jamaa za abiria waliokuwemo ndani ya ndege wamekuwa katika uwanja wa ndege wa Cairo wakisubiri habari zaidi kuhusu wapendwa wao. Miongoni mwa waliokuwemo ndani ya ndege hiyo aina ya MS804 ni raia 30 wa Misri, wafaransa 15, wairaqi 2, watoto wawili na mmoja mdogo, Uingereza, Kuwait, Ubelgiji, Saudi Arabia, Sudan, Chad, Ureno, Algeria na Canada wakiwa na raia mmoja mmoja.

Mwandishi: John Juma/APE/RTRE/AFPE/DPE

Mhariri:Josephat Charo