1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maas: Urafiki kati ya Ujerumani na Marekani si wa kupingika

Caro Robi
3 Oktoba 2018

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas anaelekea Washington, Marekani kwa mazungumzo na pia kufungua kampeni ijulikanayo kama mwaka wa urafiki kati ya Wajerumani na Wamarekani.

https://p.dw.com/p/35u9P
Heiko Maas

 Maas amesema mahusiano kati ya pande hizo mbili ni muhimu na Ujerumani inahitaji kuingia katika mazungumzo ya kina na Marekani wakati ambapo kuna tofauti kubwa kati yao na kuongeza kuwa licha ya Ujerumani na Marekani kutofautiana kuhusu karibu masuala yote ya kisiasa hivi sasa, lakini urafiki kati yao ni jambo lisilopingika.

Maas amesema Marekani inasalia kuwa mshirika muhimu zaidi wa Ulaya. Tangu Rais Donald Trump kuingia madarakani mwezi Januari mwaka jana, mahusiano kati ya Marekani na Ujerumani umekuwa tete na zinatofautiana vikali kuhusu masuala kama mpango wa kinyuklia wa Iran, matumizi ya kifedha katika jumuiya ya kujihami ya NATO na biashara.

Je, uhusiano utaboreka?

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema mambo ambayo yalikuwa yakichukuliwa kuwa ya kawaida hayako hivyo tena na yanahitaji kufanyiwa kazi akifafanua kuwa chini ya utawala wa Rais Barack Obama, kulikuwa pia na maoni na misimamo tofauti, lakini kulikuwa na mazungumzo ya mara kwa mara kati ya washirika hao wawili na chini ya uongozi wa sasa wa Marekani hayo hayafanyiki tena.

Paneldiskussion Wunderbar together in Berlin
Washiriki wa mdahalo kuhusu kampeini ya Wunderbar togetherPicha: DW/E. Grenier

Trump mara kwa mara amemkosoa vikali Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Chini ya kauli mbiu iliyopewa jina Wunderbar Together yaani 'vizuri pamoja', zaidi ya hafla 1,000 zitaandaliwa katika majimbo yote 50 ya Marekani katika kipindi cha mwaka mmoja ujao kuimarisha mahusiano kati ya Marekani na Ujerumani.

Kampeini hiyo inayolenga kuimarisha mahusiano inazinduliwa leo na itaangazia masuala ya teknolojia, mazingira, tamaduni mbali mbali, miongoni mwa masuala mengine. Ujerumani imesema lengo la kampeini hiyo sio tu kudumisha mahusiano bali kuyaboresha na kuwafanya watu kujifunza mengi zaidi kuhusu Ujerumani kuliko wanavyosikia na kuona katika vyombo vya habari.

Akiwa Marekani, Maas atakutana na mwenyeji wake waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, mshauri wa usalama wa taifa John Bolton, wabunge na maafisa wengine wa ngazi ya juu. Mbali na kutafuta kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, masuala ya Syria, Iran na Urusi yatajadiliwa.

Mwandishi: Caro Robi/https://www.dw.com/en/german-fm-heiko-maas-relations-with-us-non-negotiable/a-45732470

Mhariri: Grace Patricia Kabogo