Maangamizi ya halaiki katika kambi ya Auschwitz-Birkenau | Masuala ya Jamii | DW | 27.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Maangamizi ya halaiki katika kambi ya Auschwitz-Birkenau

Kimataifa Januari 27 ni siku ya kukumbuka maangamizi ya halaiki.Siku hiyo pia katika mwaka 1945,kambi ya Manazi ya Auschwitz-Birkenau nchini Poland ilikombolewa na vikosi vya Soviet Union.

Mauaji makubwa kabisa ya Wayahudi yalifanywa kwa mpangilio katika kambi hiyo.Kila mwaka kiasi ya watu milioni moja kutoka kila pembe ya dunia hutembelea Auschwitz kukumbuka mauaji ya Wayahudi yaliyotokea.Hiyo ni idadi kubwa ya watu wanaotaka kujionea wenyewe jinsi maisha yalivyokuwa na yalivyoteketezwa katika kambi hiyo.Lakini hivi karibuni wasimamizi wa kambi hiyo walionya kuwa majengo ya kambi hiyo yanahitaji kufanyiwa ukarabati na gharama zake ni kubwa mno.Ujerumani haikusita kutoa mchango wa fedha.Kwani hata baada ya zaidi ya miaka sitini tangu kumalizika kwa vita,nchi na jamii zina jukumu la kihistoria kuhifadhi kumbukumbu hiyo.Hata ikiwa si rahisi kufanya hivyo wakati ukizidi kupita na watu walioshuhudia mauaji hayo wakifariki.Hapo tena vitabu vya historia, nyumba za makumbusho,filamu za kuonyesha hali halisi iliyokuwepo ndio zitachukua nafasi ya masumilizi ya watu binafsi.

Kujifunza kutokana na yale yaliyotokea vile vile humaanisha kuzingatia wakati wa hivi sasa na kujiandaa dhidi ya ubaguzi,chuki ya wageni,ubaguzi wa kikabila na pia chuki ya Uyahudi.Bila shaka husikitisha kushuhudia kuwa wakati wa mivutano ya hivi karibuni kati ya Israel na Wapalestina,baadhi ya watu hawakujizuia kama kawaida yao kwani barua na barua pepe zilizojaa chuki ziliwalenga watu wenye asili ya Kiyahudi.Hayo yametokea hata Ujerumani.Kinachotisha ni kuona kuwa watu wenye chuki ya Uyahudi wanangánia msimamo wao kama uchunguzi wa maoni unavyodhihirisha mara kwa mara.

Licha ya hayo yote,siku hii ya leo ya kumbukumbu ya maangamizi ya halaiki kunafanywa mikutano na hafla mbali mbali zinazohusika na suala hilo.Jitahada ya kuhifadhi kumbukumbu hiyo ingefaa pia kuwa wajibu wa Ulaya.Ujerumani iliyopitia njia ndefu na ngumu kukabiliana na historia ya uhalifu uliotendwa na Manazi inaweza kuwa mfano kwa nchi zingine za Ulaya pia kukabiliana na ukweli wa historia zake.

 • Tarehe 27.01.2009
 • Mwandishi C.Rabitz - (P.Martin)
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GhPt
 • Tarehe 27.01.2009
 • Mwandishi C.Rabitz - (P.Martin)
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GhPt
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com