1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yazuka Uganda baada ya wabunge wawili kukamatwa

Admin.WagnerD31 Agosti 2018

Maandamano yamezuka kwenye mji mkuu wa Uganda Kampala baada ya polisi kuwazuia na kuwakamata jana wabunge wawili akiwemo Mwanamuziki maarufu wa Uganda Bobi Wine wakati walipotaka kusafiri kwenda nje ya nchi kwa matibabu.

https://p.dw.com/p/3476p
Uganda Proteste in Kampala
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Wandera

Maandamano hayo ni ya karibuni kabisa tangu taarifa za kuzuiwa na kushikiliwa wanasiasa hao wa upinzani ziliposambaa jana usiku wakati wabunge hao walipojaribu kwa wakati tofauti kuabiri ndege kwenda nje ya nchi kwa lengo la kupatiwa matibabu.

Wote wawili wanatafuta matibabu nje ya nchi baada ya kudai kuwa waliteswa na kuumizwa walipokamatwa na walipokuwa kwenye kizuizi cha jeshi, madai ambayo serikali imeyakanusha.

Waandamanaji kwenye maeneo tofauti ya mji mkuu Kampala, wamechoma moto tairi za magari na kurusha mawe pamoja na kuweka vizuizi katikati ya barabara.

Dick Nyule ambaye ni mwandishi habari wa kituo kimoja cha radio nchini Uganda ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa maandamano yalikuwa makubwa kwenye kitongoji cha Kamwokya mjini Kampala eneo ambalo Kyagulanyi anamiliki studio ya kurekodia muziki.

Polisi imesema hata hivyo kuwa imefanikiwa kuyadhibiti na kuyazima maandamano hayo. Msemaji wa polisi Emilian Kayima amesema askazi polisi walitawanywa kwenye kitongoji cha Kamwokya kutokana na baadhi ya vijana kutaka kuzusha taharuki.

Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine ilikuwa asafiri kwenda marekani na mwenzake Francis Zaake alikuwa anasafiri India wakati polisi ilipowakamata kwa nguvu katika uwanja wa ndege wa kimaaifa wa Entebbe.

Tangu wakati huo wanasiasa hao wamezuiliwa katika hospitali moja ya serikali mjini Kampala na polisi imesema watapatiwa matibabu chini ya uangalizi wa polisi.

Bobi Wine huenda akafunguliwa mashtaka mengine

Asumani Basalirwa ambaye ni mmoja wa mawakili wa Bobi Wine ameiambia DW kuwa afya ya mwanasiasa huyo bado ni tete na polisi imewaarifu kuwa inalenga kumfungulia mashtaka mengine na huenda akafikishwa mahakamani jumatatu ya wiki ijayo.

Bobi Wine tayari anakabiliwa na mashtaka ya uhaini baada ya kutuhumiwa kushiriki vurugu zilizosababisha msafara wa Rais Yoweri Museveni kushambuliwa kwa mawe katikati ya mwezi Agosti.

Uganda Sänger Bobi Wine
Picha: DW/E. Lubega

Basalirwa amesema polisi haijatoa maelezo yoyote ya ziada kuhusu madai hayo mapya na kusisitiza wanafanya kazi kubwa kuhakikisha mbunge huyo anaachiwa kutoka kizuizi cha hospitalini.

Msemaji wa serikali Ofwono Opondo amesema mbunge Zaake, ambaye hajafunguliwa mashitaka yoyote ya uhalifu  alitoroka kutoka kizuizi cha polisi na alipaswa kukamatwa haraka iwezekanavyo.

Serikali inataka taarifa zao za afya

Kadhalika polisi imesema ilikuwa inahitaji taarifa ya madaktari kwa sababu wabunge hao wamesema waliteswa walipokuwa kizuizini lakini maafisa wa hospitali wamekataa kushirikina na polisi kupata maelezo ya wanaiasa hao .

Kulingana na asasi moja ya haki za binadamu nchini humo Kyagulanyi na Zaake wamekuwa wakizuia hatua ya wataalam wa afya waliopelekwa na  serikali kuwafanyia uchunguzi.

Wakili wake mwingine Nicholas Opiyo amesema kushikiliwa kwake ni kinyume cha utaratibu na amezituhumu mamlaka nchini Uganda kwa kujaribu kutengeneza taarifa zao wenyewe juu ya afya ya Bobi wine ili kuficha ushahidi wa mateso na majeraha aliyopata.

Uganda «Präsident der Ghettos» Bobi Wine wegen Hochverrats angeklagt
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Kabuubi

Bobi Wine  ni miongoni mwa kundi la wabunge watano waliokamatwa katikati ya mwezi Agosti katika mji wa kaskani magharibi wa Arua kwa tuhuma za kuushambulia kwa mawe msafara wa Rais Yoweri Museveni wakati wa mkutano wa kampeni wa uchaguzi mdogo wa ubunge.

Bobi Wine ambaye alishinda kiti cha ubunge kama mgombea binafsi mwaka uliopita ameibuka kuwa mwanasiasa wa upinzani mwenye nguvu na na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Yoweri Museveni anayehofiwa kutaka kutawala zaidi, baada ya kuwa madarakani kwa miaka 32.

Mwandishi : Rashid Chilumba/Reuters/APE

Mhariri: Iddi Ssessang