1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yanaendelea huko Congo kumpinga Malonda

Jean Noel Ba-Mweze13 Julai 2020

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baadhi ya Wakongomani kutoka upinzani pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za raia tayari wanaandamana katika baadhi ya miji ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3fE5Z
Demonstrationen gegen die Präsidentschaftspartei Union für Demokratie und sozialen Fortschritt (UDPS) in Kinshasa
Picha: Getty Images/AFP/A. Mpiana

Maandamano hayo yameandaliwa na upinzani ili kupinga kuthibitishwa kwa Ronsard Malonda, kama mwenyikiti wa tume huru ya uchaguzi nchini humo, ingawa serikali imeyazuia maandamano yoyote kwa lengo la kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 unaoikumba Kongo.

Polisi tayari wamejipanga kila mahali kando ya makao makuu ya bunge la taifa, ili kuwazuwia waandamanaji wasifanikiwe kujipenyeza katika makao hayo. Miongoni mwa waandamanaji kutoka upinzani ni wanachama wa MLC chama cha Jean-Pierre Bemba, wale wa Ensemble pour la Republique chama cha Moses Katumbi na wafuasi wengine wa upinzani. Baadhi ya wanaharakati wa kutetea haki za raia wapo pia barabarani ili kupinga kuthibitishwa kwa Ronsard Malonda, kama mwenyikiti wa tume huru ya uchaguzi.

Demonstrationen gegen die Präsidentschaftspartei Union für Demokratie und sozialen Fortschritt (UDPS) in Kinshasa
Polisi wakipita kando ya jengo linalowaka moto mjini KinshasaPicha: Getty Images/AFP/A. Mpiana

Serikali imepiga marufuku maandamano yote na ndiyo maana polisi wamesambazwa kila mahali mjini Kinshasa. Ama kwa upande mwengine, naibu waziri mkuu anayehusika na sheria, Celestin Tunda ya Kasende ambaye ni  mwanachama wa FCC, chama cha rais wa zamani wa Kongo, Joseph Kabila, alijiuzulu siku ya Jumamosi baada ya mgogoro na Rais Felix Tshisekedi. Mgogoro huo ulitokana na Tunda kutowa maoni kwenye bunge kwa niaba ya serikali, ili kuunga mkono miswada ya kuleta mageuzi katika sekta ya sheria, ingawa hakulijulisha baraza la mawaziri.

Na kama ilivyokuwa ikitarajiwa na wengi, Celestin Tunda ya Kasende kajiuzulu, ila kajisifu kwa juhudi na kazi alizozifanya kwa kuitii sheria ya nchi hii. Celestin Tunda ya Kasende anasema;

''Siyo kama sikustahili, ila kwa unyenyekevu, naondoka serikalini nikiamini kwamba kazi yangu katika wizara ya sheria, ilisaidia kabisa kuimarisha utii wa sheria nchini mwetu.''

Demonstrationen gegen die Präsidentschaftspartei Union für Demokratie und sozialen Fortschritt (UDPS) in Kinshasa
Maafisa wa polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini KinshasaPicha: Getty Images/AFP/A. Mpiana

Mambo yanaendelea kuzorota kati ya muungano wa CACH, wa Rais Tshisekedi na FCC, muungano wa kabila. Aidha, chama cha UDPS, cha Rais Tshisekedi, kimewaonya mawaziri wengine na wauzingatie mfano wa Kasende, ili kurekebisha mwenendo wao na kufanya kazi kwa unyenyekevu. Yusuf Mabanze ni mmoja wa viongozi wa UDPS.

''Hilo ndilo lilimfikia Tunda ya Kasende. Ilionekana ya kwamba alikiuka masharti na vipengele vinavyoiongoza serikali ya Kongo. Tuna matumaini kwamba hiyo ni jambo la kuwakumbusha mawaziri wote kufanya kazi yao kwa unyenyekevu kwa rais na kutii sheria za nchi.''

Katika hotuba yake, aliyoitoa mwishoni mwa mwezi uliopita wakati wa kuahdimisha miaka sitini ya uhuru wa Kongo, Rais Tshisekedi alisema hatafanya mageuzi yatakayolenga kuharibu uhuru wa mamlaka ya sheria. Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.

Jean Noel Ba-Mweze-DW Kinshasa