1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yaendelea Mnyanmar kushinikiza utawala wa kiraia

Amina Mjahid
10 Februari 2021

Makundi makubwa yanayopinga jeshi la Mnyanmar kuchukua madaraka, yameendelea kuandamana licha ya marufuku ya kutoandamana kuwekwa, huku vikosi vya usalama vikitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji

https://p.dw.com/p/3pAsA
Myanmar Proteste | Ausgangssperre und Versammlungsverbote
Picha: AP Photo/picture alliance

Walioshuhudia wanakadiria kuwa maelfu ya waandamanaji walijitokeza katika miji ya Yangoon na Mandalay, ambayo ni miji mkubwa nchini humo. Maandamano mengine pia yalishuhudiwa katika mji wa  Naypyitaw na maeneo mengine katika taifa hilo.

Waandamanaji wanataka utawala wa kiraia urejeshwe kwa serikali ya Aung Sang Suu Kyi, na pia wanataka kiongozi huyo na viongozi wengine wa chama chake waachiwe huru, tangu walipokamatwa baada ya jeshi kuzuwia bunge jipya kukutana mnamo februari mosi.

Baadhi ya waandamanaji mjini Yangoon walikusanyika katika balozi za kigeni wakitaka uungwaji mkono wa kimataifa kushinikiza jeshi kurejesha utawala wa kidemkorasia.

Myanmar Proteste | Ausgangssperre und Versammlungsverbote
Kiongozi wa jeshi Myanmar Jenerali Min Aung Hlaing Picha: Myawaddy/AP Photo/picture alliance

Kundi dogo katika ubalozi wa Japani ulibeba mabango yanayosema "tunataka demokrasia, lakini badala yake tunapata madikteta" wengine walionekana wakibeba bendera za chama cha Suu Kyi na wengineo nao wakibeba jeneza wakiashiria kuwa ni maziko ya Jenerali Ming Aung Hlaing aliyeongoza mapinduzi na kuchukua madaraka.

Hata hivyo Jeshi limesema limechukua uamuzi wa kuipindua serikali kutokana na madai kwamba uchaguzi wa Novemba uliokipa ushindi chama cha Suu Kyi, ulikumbwa na udanganyifu, madai ambayo tume ya uchaguzi imeendelea kuyakanusha.

Jeshi hapo jana lilivamia makao makuu ya chama cha Suu Kyi ambapo kabla ya jeshi kuchukua madaraka kiongozi wao alikuwa aapishwe kwa muhula wa pili wa miaka mingine mitano madarakani baada ya kushinda uchaguzi wa Novemba. Msemaji wa chama hicho aliandika katika ukurasa wa facebook kwamba jeshi lilivamia makao makuu yake na kuchukua stakabadhi na compyuta kadhaa.

Uvamizi katika makao makuu ya chama cha Suu Kyi wakosolewa vikali

Marekani imekosoa vikali uvamizi huo na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji, ikiitaka pia jeshi kurejesha utawala wa kiraia, kuwaachia huru waliokamatwa na kutodhibiti mawasiliano.

Myanmar Proteste gegen den Militärputsch
Picha ya Kiongozi wa chama cha kisiasa cha NLD Aung San Suu KyiPicha: Reuters

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani amesema taifa hilo linafuatilia kwa makini kile kinachoendelea na huenda, Marekani ikatafakari upya msaada inayotoa kwa Mnyanmar ili wale waliohusika na mapinduzi wachukuliwe hatua kali.

Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya haki za binaadamu lililo na wanachama  47 litakutana mjini Geneva siku ya Ijumaa kuangalia athari ya ukiukwaji wa haki za binaadamu katika mgogoro wa Myanmar.

Uingereza na Umoja wa Ulaya kwa upande wao wametaka kuharakishwa kwa mkutano huo wa Ijumaa utakaozua mjadala mkubwa juu ya mgogoro huo wa Myanmar na huenda ukatoa majibu ya kimataifa dhidi ya yale yanayoendelea nchini humo.

Tayari mkuu wa masuala ya diplomasia katika Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema umoja huo unatafakari kuliwekea vikwazo jeshi la Myanmar.

Vyanzo: ap/dpa/Reuters