1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya mabadiliko ya tabia nchi yafanyika Kenya

Amina Mjahid
20 Septemba 2019

Wanaharakati nchini Kenya wameungana na ulimwengu kuandamana kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Wanaharakati hao wanasema kuwa pana haja ya serikali nchini humo kukuza matumizi ya nishati safi kwa sababu ya vizazi vijavyo.

https://p.dw.com/p/3Px9m
BG FFF weltweit | Kenia| Klimastreik | Global Strike 4 Climate | Nairobi
Picha: DW/S. Wasilwa

Maandamano haya yaliyoanzia katika eneo la Freedom Corner, linalohusishwa na marehemu profesa Wangari Maathai, mshindi wa tuzo ya nobel ya mazingira, yameshirikisha zaidi ya vijana elfu moja waliokuwa wamevalia fulana nyeupe na nyekundu pamoja na mabango yenye maandishi kuhusu mazingira.

Yanajiri wakati serikali ikipanga kuwaondoa watu waliouvamia msitu wa Mau ambao ni moja ya vyanzo vikuu vya maji nchini Kenya.

"Kwa hivyo lazima tuwe na wasiwasi. Lazima tuhifadhi vyanzo vyetu vya maji, misitu yetu…Lazima tuhakikishe tunaacha sayari ambayo inaweza kuhifadhi kizazi kijacho sio tu sisi,” alisema Houghton Irungu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Amnesty International nchini Kenya.

Ripoti zinaonesha kuwa kwa kipindi cha kati ya miaka 50 na 100 iliyopita, hali joto katika maeneo mengi brani Afrika iliongezeka kwa asimilia 0.5 na inatarajiwa kuongezeka kwa kasi katika karne hii ya 21.

Viwango vya joto vyaongezeka katika baadhi ya maeneo Kenya

BG FFF weltweit | Kenia| Klimastreik | Global Strike 4 Climate | Nairobi
Picha: DW/S. Wasilwa

Taswira hiyo imeonekana nchini Kenya huku maeneo mengi kama vile Murang'a ambayo huwa yana baridi yakirekodi halijoto ya nyuzi 34. Mapema mwaka huu, wataalam wa hali ya hewa waliwaonya wakazi wa Nairobi kutulia nyumbani kuanzia saa sita mchana hadi saa tisa kwa sababu ya joto kubwa.

"Leo nimekuja kuungana na vijana wenzangu kuhusu hii maandamano ya mabadiliko ya tabianchi, kwa sababu jinsi wanasayansi wametuambia katika ripoti ya IPPC, tuko na takriban miaka 10, kuanzia leo ambapo ikishatimia miaka hiyo hatutaweza kuyarebisha mabadiliko ya tabianchi,” alisema mmoja ya vijana walioshiriki maandamano hayo, Dolphine Magero.

Aidha kilimo ambacho ndio uti wa mgongo kimeathiriwa katika siku za hivi karibuni na ukame na kiangazi cha muda mrefu. Ithibati ya athari zake ni maafa ambayo yaliripotiwa katika jimbo la Turkana. Maandamano ya vijana hawa yaliishia katika wizara ya nishati ambapo waliwasilisha ombi lao kwa waziri husika.

Aidha wanaharakati hawa wanaitaka serikali ya Kenya kusitisha mpango wake wa kuanzisha kiwanda cha makaa ya mawe na kuchunguza visa vya ufisadi katika miradi ya mabwawa nchini.

Chanzo: DW Nairobi.